• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 24, 2016

  UGENI, UTOVU WA NIDHAMU WA VIONGOZI WAKE VILIWAPONZA YANGA KUVURUNDA KOMBE LA SHIRIKISHO

  MABINGWA wa Tanzania, Yanga SC jana wamehitimisha mechi zao za Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 3-1 na wenyeji TP Mazembe, Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, DRC.
  Kwa matokeo hayo, Mazembe inamaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake 13 baada ya mechi sita, wakati Yanga inamaliza mkiani kwa pointi zake nne. 
  MO Bejaia ya Algeria iliyomaliza na pointi nane sawa na Medeama ya Ghana, inaungana na Mazembe kwenda Nusu Fainali.
  Hiyo ni kwa sababu Bejaia ilipata matokeo mazuri ya jumla dhidi ya Medeama, ikitoa sare ugenini na kushinda 1-0 nyumbani.
  Yanga jana ilicheza pungufu tangu dakika ya 30, baada ya beki wake chipukizi, Andrew Vincent Chikupe ‘Dante’ kutolewa kwa kadi nyekundu.
  Beki huyo aliyesajiliwa Mei mwaka huu kutoka Mtibwa Sugar alitolewa dakika mbili tu baada ya Mazembe kupata bao la kwanza lililofungwa na Jonathan Bolingi, aliyemalizia pasi ya Deo Kanda.
  Wakati Yanga SC wakikianza kipindi cha pili kwa kasi ya kusaka bao la kusawazisha, Mazembe wakafanikiwa kupata bao la pili, lililofungwa na Ranford Kalaba dakika ya 55 kabla ya Bolingi kufunga la tatu dakika ya 64.
  Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga SC bao la kufutia machozi dakika ya 75 – hilo likiwa bao la nne la timu hiyo kwenye mashindano hayo.
  Katika mabao hayo manne, Tambwe amefunga mawili, lingine kwenye mechi na MO Bejaia, wakati Mzimbabwe Donald Ngoma alifunga dhidi ya Medeama Dar es Salaam na mzalendo Simon Msuva akafunga kwa penalti nchini Ghana.
  Yanga ilianza michuano hiyo kwa kufungwa 1-0 na MO Bejaia nchini Algeria, kabla ya kufungwa 1-0 tena na Mazembe na baadaye sare ya 1-1 na Medeama ya Ghana, mechi zote zikipigwa Dar es Salaam.
  Katika mzunguko wa pili, Yanga ikafungwa 3-1 na Medeama nchini Ghana, kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Mo Bejaia Dar es Salaam na leo kupigwa 3-1 Lubumbashi.  
  Ukitazama matokeo ya jumla ya Kundi A, unaweza kabisa kuiponda Yanga kwamba imevurunda – lakini ukienda kwenye tathmini za kitaalamu na kufanya upembuzi yakinifu, utagundua timu ya Tanzania ilijitahidi.
  Kwa sababu kwanza Yanga ndiyo ilikuwa timu duni zaidi katika Kundi A na kwa ujunla kwenye hatua yote ya makundi, ambayo inafuzu kwa mara ya kwanza kwenye hatua ya makundi ya michuano hiyo.
  Na bahati mbaya viongozi wake wakafanya uzembe kwa kutohudhuria semina ya mwongozo wa ushiriki wao mashindano hayo mjini Cairo, Misri.
  Hiyo iliwaathiri Yanga wakajikuta wanacheza baadhi ya mechi katika muda na siku ambazo hawakutaka wao, hivyo kuvuruga programu za benchi la Ufundi tu kwa kutofahamu utaratibu wa kuitaarifu mapema CAF siku na muda wa mchezo.
  Walionekana kuanza vizuri, baada ya kwenda kuweka kambi ya wiki moja Uturuki na wakaenda kucheza vizuri wakifungwa 1-0 ugenini na MO Bejaia.  
  Lakini mchezo dhidi ya TP Mazembe Dar es Salaam kuna kitu Yanga walikosea katika maandalizi yao – kwanza timu ilirudi hapa siku tano kabla ya mechi baada ya kambi ya Uturuki, wakati ilitarajiwa kurejea siku moja kabla ya mechi.
  Na walipofika Dar es Salaam inadaiwa kwa siku mbili walikosa Uwanja wa kufanyia mazoezi, jambo ambalo liliathiri maandalizi katika siku za mwishoni.
  Viongozi nao wakaingia kwenye malumbano yasiyo na tija na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na kujikuta wanacheza mechi ya nyumbani kama wapo ugenini na wakafungwa 1-0.
  Kitendo cha kuendelea kutunishiana misuli na TFF hakika kiliwaponza wakashindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Medeama Dar es Salaam, ambayo yangewatia nguvu hata ya kwenda kupigania matokeo mazuri mengine ugenini.
  Yanga walitoa sare ya 1-1 hapa nyumbani na kupoteza matumaini ya kwenda Nusu Fainali – lakini baada ya Mo Bejaia kubanwa na Mazembe kwa sare nyumbani, nafasi ya pili ya kundi ikawa bado ipo wazi.
  Na Yanga wakaenda Ghana kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Medeama kujaribu kushinda, bahati mbaya wakafungwa 3-1, ingawa pia kwa Mo Bejaia kufungwa na Mazembe Lubumbashi, nafasi ya pili ikawa bado iko wazi.
  Yanga wakapata ushindi wa kwanza wa mashindano nyumbani, wakiifunga 1-0 MO Bejaia Dar es Salaam na kufufua matumaini ya kwenda Nusu Fainali, lakini ushindi wa 3-2 wa Medeama dhidi ya Mazembe Ghana ukazima ndoto hizo.
  Na jana mechi za Kundi A zimehitimishwa, Yanga ikishika mkia, Medeama ya tatu, Bejaia ya pili Mazembe vinara wa kundi.
  Huu ndiyo hata mimi ulikuwa utabiri wangu mapema tu, kwamba Mazembe itaongoza kundi ikifuatiwa Bejaia, Medeama na Yanga itashika mkia – labda itokee miujiza.
  Nilichotazama ni uwezo wa timu na uwekezaji wake ndiyo nikatarajia hivyo, kwa kuwa mimi ni muumini wa uwezo pamoja na kuheshimu jitihada.
  Sifikirii kama ni sahihi kuanza kuiponda Yanga baada ya kushika mkia Kundi A, zaidi ya kuwaonyesha kwanza walijikwaa wapi.
  Kikubwa Yanga iliponzwa na ugeni uliowafanya wakose uzoefu wa kucheza mashindano makubwa kama hayo pamoja na ukosefu wa nidhamu wa uongozi wake, chini ya Mwenyekiti, Yussuf Manji.
  Nidhamu mbovu iliyowafanya wakashindwa kuhudhuria mafunzo ya CAF mjini Cairo na pia kuingia kwenye malumbano yasiyo na tija na TFF.
  Ndiyo maana wameburuza mkia Kundi A, wakiambulia kushinda mechi moja tu na kwa kujumla kuvuna pointi nne tu nyumbani. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UGENI, UTOVU WA NIDHAMU WA VIONGOZI WAKE VILIWAPONZA YANGA KUVURUNDA KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top