• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 23, 2016

  SERIKALI YAFIKIRIA KUSAIDIA KAMBI YA SERENGETI BOYS DHIDI YA KONGO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye amesema Serikali itaangalia uwezekano wa kusaidia maandalizi ya timu ya vijana chini ya umri wa miaak 17, Serengeti Boys kabla ya mchezo wao dhidi ya Namibia mwezi ujao.
  Nape alikuwepo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Jumapili wakati Serengeti Boys inaifunga Afrika Kusini mabao 2-0 na kufuzu hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Fainali za U-17 Afrika mwakani Madagascar na baada ya mechi akatoa ahadi hiuyo.
  Nape alimuambia Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliyekuwa naye jirani jukwaani kwamba Serikali wataangalia uwezekano wa kushirikiana na TFF kusaidia kambi ya timu kwa maandalizi ya mchezo wa Namibia.
  Waziri Nape akifurahia na Rais wa TFF, Jamal Malinzi Jumapili Chamazi

  Kwa upande wake, Malinzi akasema Serengeti Boys itaingia kambini Septemba 1 nje ya nchi ambako watakaa kwa wiki mbili kujiandaa na mechi dhidi ya Kongo Brazaville. “Kwa sasa wanavunja kambi kwa wiki moja, tutafahamishana kwa undani zaidi mipango ikikamilika,”alisema Malinzi.
  Serengeti Boys imefuzu kwa ushindi wa jumla wa 3-1 baada ya sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Afrika Kusini na katika hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi ya Madagascar mwakani watamenyana na Kongo Brazaville iliyoitoa Namibia.
  Pongezi kwa wafungaji wa mabao hayo Jumapili, Mohamed Rashid Abdallah kipindi cha kwanza na Muhsin Malima Makame kipindi cha pili katika mchezo ambao Serengeti Boys ililazimika kucheza pungufu tangu dakika ya 44 baada ya kiungo wake wa ulinzi, Ally Hamisi Ng’anzi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu.
  Serengeti Boys ilipata bao lake la kwanza dakika ya 34 baada ya Mohamed Rashid Abdallah kumalizia vizuri pasi ya Yohana Nkomola kumtungua kipa wa Amajimbos Glen Tumelo Baadjes.
  Benchi la Ufundi la Serengeti Boys, chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mdenmark Kim Poulsen, Kocha Mkuu, Bakari Shime na Kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’, lilirudi na mipango mizuri kipindi cha pili na timu ikaendelea kutawala mchezo licha ya kucheza pungufu na haikuwa ajabu Makame alipofunga bao la pili dakika ya 83 kwa shuti akimalizia krosi ya Mohamed Rashid Abdallah.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERIKALI YAFIKIRIA KUSAIDIA KAMBI YA SERENGETI BOYS DHIDI YA KONGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top