• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 26, 2016

  SAMATTA: TUMEPANGWA NA TIMU ZENYE UZOEFU WA MICHUANO YA ULAYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba anajisikia furaha kwa kuiwezesha timu yake kufika hatua ya makundi ya Europa League, lakini wamepangwa kundi gumu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo usiku, Samatta amesema kwamba kufika hatua ya makundi kunazidi kumpatia uzoefu na ana imani itazidi kumuongezea ubora kiuchezaji.
  KRC Genk imepangwa Kundi F pamoja na Athletic Bilbao ya Hispania, Rapid Vienna ya Austria na Sassuolo ya Italia katika Europa League.
  Samatta amesema kwamba anajisikia furaha kwa kuiwezesha timu yake kufika hatua ya makundi ya Europa League

  Na hiyo ni baada ya Samatta kufunga bao la kwanza la Genk ikishinda 2-0 na kufuzu hatua ya makundi ya Europa League usiku wa Alhamisi katika mchezo huo wa marudiano hatua ya mwisho ya mchujo dhidi ya Lokomotiva Zagreb ya Croatia Uwanja wa Luminus Arena, Genk dakika ya pili tu akimalizia pasi ya Mjamaica, Leon Bailey.
  Na ni Bailey ndiye aliyeifungia Genk bao la pili dakika ya 50 katika mchezo ambao Samatta alimpisha Mgiriki Nikolaos Karelis dakika ya 80 na timu hiyo inafuzu kwa ushindi wa jumla wa 4-2 baada ya sare ya 2-2 katika mchezo wa kwanza.
  Nahodha huyo wa Tanzania, Alhamisi ya wiki iliyopita alifunga pia bao moja KRC Genk ikitoa sare ya 2-2 Uwanja wa Maksimir mjini Zagreb.
  Na katikati ya mechi hizo, Samatta alifunga mabao mawili Genk ikishinda 3-0 dhidi ya wenyeji, Lokeren Uwanja wa Daknam mjini Lokeren Jumapili katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji.
  Akilizungumzia kundi hilo, Samatta alisema; “Kundi linaonekana kama rahisi, lakini siyo rahisi, timu zote ni timu zenye uzoefu wa mashindano ya Ulaya, wamekuwa washiriki karibu kila mwaka, kwa hiyo binafsi nategemea kukutana na upinzani mkali katika hatua hiyo ya makundi,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA: TUMEPANGWA NA TIMU ZENYE UZOEFU WA MICHUANO YA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top