• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 25, 2016

  MORO KIDS WATWAA UBINGWA WA AIRTEL RISING STARS WA MKOA 2016

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya vijana ya Moro Kids imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya Airtel Rising Stars baada ya kufanya kazi ya ziada na kuishinda timu ngumu ya Angrikana 1-0 katika mchezo wenye upinzani mkali uliochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro jana.
  Goli hilo la ushindi liliwekwa kimiani na mshambuliaji machachari Nyamawi Juma katika dakika ya 22 baada ya kuwazidi mbio walinzi wa Angrikana na kuachia shuti kali lililotinga wavuni. Goli liliibua nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki waliojitokeza kwa wingi kushangilia timu yao. 
  Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga akimkabidhi Kapteni wa timu ya Moro Kids, Abdul Rashid Kombe la ubingwa wa mashindano ya Airtel Rising Stars mkoani humo baada ya kuifunga timu ya Angrikana 1-0 
  Wachezaji wa Moro Kids wakishangilia baada ya kuifunga timu ya Angrikana 1-0 katika uwanja wa Jamhuri Morogoro 

  Angrikana walijibu mapigo kwa kufanya mashambulizi mfululizo ambayo hata hivyo hayakuweza kuzaa matunda. Kipingi cha pili walikianza kwa matumaini ya kupata goli la kusawazisha lakini hadi dakika ya mwisho matokeo yalibaki kuwa 1-0. 
  Akikabidhi kikombe kwa washindi, Meya wa manispaa ya Morogoro Pascal Kihanga ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwapongeza Morogoro Kids kwa mafanikio makubwa na kuwataka kuendelea kufanya mazoezi kwa kujituma huku wakifuata maelekezo ya walimu wao. “Kwa kufanya hivyo kutawaweka katika nafasi nzuri ya kutimiza ndoto zenu za kufanikiwa katika maisha kupitia soka”, alisema. 
  Aliwataka viongozi wa soka mkoani Morogoro pamoja na makocha kuhakikisha wanachagua vijana wenye vipaji ili kuuwakilisha vyema mkoa wa Morogoro kwenye fainali za taifa za Airtel Rising Stars zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 6 hadi to 11.
  Wakati wa mechi hizo za mkoa makocha walipata fursa ya kuwatathimini uwezo wa kila mchezaji na kuchagua vijana wenye vipaji kuunda kombaini ya mkoa. Mikoa mingine ambayo tayari imeshaunda vikosi vyake ni kwa fainali hizo ni Ilala, Kinondoni, Temeke and Mwanza.
  Fainali hizo za kila mwaka itazikutanisha timu za wavulana na wasichana kutoka mikoa ya kisoka ya Ilala, Kinondoni na Temeke. Washiriki wengine watatoka Mwanza, Morogoro, Mbeya, Lindi, Arusha na Zanzibar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MORO KIDS WATWAA UBINGWA WA AIRTEL RISING STARS WA MKOA 2016 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top