• HABARI MPYA

    Sunday, August 28, 2016

    DILILI ZA TFF KUFELI MAPEMA KUPATA KIKOSI CHA OLIMPIKI YA TOKYO 2020?

    MOJA kati ya mambo yanayomfanya Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi aonekane kiongozi tofauti na wengi nchini ni namna alivyo mwepesi kushiriki mijadala.
    Malinzi anashiriki kwa wingi mijadala ya maendeleo ya soka na michezo kwa ujumla nchini.
    Amejishirikisha hadi katika makundi mengi ya mijadala kwenye makundi ya mitandao ya jamii, mfano Whatsapp  na anatoa na kuchangia sana mada kupitia akaunti yake ya Twitter.
    Wiki hii Malinzi ameandika makala nzuri ya baada ya Michezo ya Olimpiki mwaka 2016 iliyomalizika mjini Rio de Jeneiro, Brazil wiki iliyopita huku Tanzania kwa mara nyingine ikirejea mikono mitupu.
    Malinzi akaandika kwamba; mwisho wa Olimpiki ya mwaka huu Rio, ndiyo mwanzo wa maandalizi ya Olimpiki nyingine ya mwaka 2020 mjini Tokyo, Japan.
    Akasema kuna mambo matatu Tanzania inatakiwa kufanya kuhusu maandalizi ya MIchezo ya Olimpiki mwaka 2020 Tokyo.
    Kwanza ni maandalizi ya TFF kwa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 (U-23)  kufaulu kushiriki fainali za Olimpiki 2020.
    Pili, ili timu ya soka na wanamichezo wengine wafaulu kushiriki na kushinda Medali za Olimpiki, zinahitajika fedha za maandalizi.
    Kuhusu soka, Malinzi akasema TFF imeamua kuanza maandalizi ya mapema yenye kuonyesha matumaini ya kufuzu kucheza Olimpiki ya 2020 katika nafasi tatu za Afrika.
    Akasema Desemba mwaka huu kutokana na ligi ya Taifa ya klabu za vijana chini ya umri wa miaka 20 inayoanza mwaka huu, watakusanya kikosi cha awali cha timu ya Taifa U23 itakayoingia kambini.
    Alisema hao ni vijana waliozaliwa baada ya Januari 1, mwaka 1997 na utatumika utaratibu ule ule ulioutumia kuijenga timu imara ya U-17, Serengeti Boys kuhakikisha wanapata mazoezi, kambi na mechi za kimataifa za kujipima.
    Akasema kufikia mwaka 2019 Tanzania itakuwa na kikosi imara cha soka mwenyewe akikiita “a world beating team” kitakachofuzu Olimpiki ya mwaka 2020.
    Hakuishia hapo, Malinzi pia nakashauri kuhusu michezo mingine akisema kwenye biashara kuna kitu kinaitwa niche. Akasema tuangalie ni eneo gani Mungu ametupa karama kuliko binadamu wengine kisha tuweke nguvu hapo.
    Akasema Tanzania tuna uwezo mkubwa wa asili kwenye michezo ya kukimbia, kuogelea, ngumi, kurusha mkuki na kurusha tufe. 
    Akashauri tunapaswa kuamua kuwekeza kwenye kuandaa watu wa kwenda kucheza michezo hiyo Tokyo mwaka 2020 ili watuletee Medali.
    Akasema tunapaswa kuanza kusaka vipaji kuanzia mwezi Desemba mwaka huu ili hadi kufika Juni mwakani tuwe na vijana wa kuanzia na tuwatafutie kambi nje ya nchi.
    Makala hii inazidi kuuanisha uanamichezo na uzalendo wa Malinzi kwa taifa lake – lakini mimi nina maswali  ya kuwauliza wao TFF kuhusu mkakati wa kwenda Olimpiki 2020 Tokyo.
    Mei mwaka huu, kampuni ya Azam Media Limited iliingia Mkataba na TFF wenye thamani ya Sh. Bilioni 2 kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania na Ligi Kuu ya Vijana wa umri chini ya miaka 20.
    Mkataba huo ulisainiwa makao Makuu ya Azam Media, eneo la TAZARA, Dar es Salaam upande wa TFF ukiwakilishwa na Rais wake, Jamal Malinzi na Azam Media wakiwakilishwa na aliyekuwa Mtendaji wake Mkuu, Muingereza Rhys Torrington ambaye ameondoka baada ya kumaliza Mkataba.
    Baada ya kusaini Mkataba huo, Malinzi alisema kwamba Ligi Kuu ya Wanawake itaanza kwa kushirikisha klabu 10 Agosti mwaka huu na Ligi ya U-20 itashirikisha klabu zote za Ligi Kuu ya Wanaume.
    Alisema Ligi ya U-20, ambayo itakuwa yenye kanuni madhubuti, itachezwa sambamba na Ligi Kuu ya wanaume, kabla ya mechi za timu za wakubwa, zitatangulia mechi za vijana na kwamba kila timu itasafirisha timu yake ya vijana kwa mechi za mikoani. 
    Malinzi amesema Ligi ya Wanawake itaanza na timu 10 baada ya hapo Chama Cha Soka ya Wanawake (TWFA) kitatengeneza muundo wa timu kupanda na kushuka.
    Kuhusu Ligi ya vijana, Malinzi amesema wataunda kanuni kali za Ligi Kuu kuhakikisha klabu zote za ligi hiyo zinashiriki kikamilifu na kwamba klabu itakayoshindwa kuingiza kikosi cha vijana uwanjani itakatwa pointi tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara  
    Malinzi amesema kila klabu ya Ligi Kuu itawajibika kuwa na timu ya U20 kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa mashindano haya zitatungwa na TFF na Ligi hizi zitaanza msimu wa 2016/2017.
    Wakati wa kusaini Mkataba, Malinzi alisema Ligi ya Wanawake itaanza Agosti na Ligi ya U-20 itaanza sambamba na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambayo ilianza wiki iliyopita.
    Lakini hadi leo siyo tu hakuna ligi iliyoanza kati ya hizo, ya U-20 na ya Wanawake bali pia hata ratiba zake hazijatoka.
    Na mkakati wa TFF kupata timu ya Olimpiki ya 2020 unaanzia kwenye Ligi ya U-20, ambayo imeanza kusuasua mapema. Tuseme hizi ni dalili za TFF kushindwa mapema kupata timu ya kufuzu Olimpiki ya Tokyo? Nauliza tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DILILI ZA TFF KUFELI MAPEMA KUPATA KIKOSI CHA OLIMPIKI YA TOKYO 2020? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top