• HABARI MPYA

  Wednesday, January 21, 2015

  ZFA WABURUZANA MAHAKAMANI TENA

  Na Abdulhafidh Habib, ZANZIBAR
  KESI ya madai ya ubadhirifu wa fedha na kuendesha shughuli za Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) inayowakabili viongozi wa juu wa chama hicho, imechukua sura mpya baada ya wadai katika kesi hiyo kuwasilisha mahakamani ombi la ukiukwaji wa amri ya mahakama.
  Ukiukwaji huo wa amri ya mahakama umedaiwa kufanywa na uongozi wa ZFA ngazi ya wilaya kwa kufanya uchaguzi uliozuiliwa na mahakama kuu.
  Ombi hilo liliwasilishwa na Makamu Rais wa  ZFA Taifa-Unguja Haji Ameir Haji pamoja na Kamati inayojiita ya mabadiliko ya Katiba ya ZFA (KK7), kupitia Mawakili wake wa kujitegemea, ambalo linapinga amri hiyo halali ya mahakama.
  Rais wa ZFA, Ravia Idarous kulia akiwa na Rais wa zamani wa caham hichi, Ali Ferej Tamim katikati na kocha mkongwe visiwani Zanzibar, Shaaban Ramadhan kushoto

  Ombi hilo lilizua mvutano wa kisheria baina ya pande mbili mahakamani hapo huku upande wa wadaiwa ukidai haujapata ombi hilo  walilotakiwa kujibu kwa maandishi.
  Hata hivyo, baada ya mvutano huo uliomlazimu Jaji Mkusa Isaac Sepetu kuakhirisha kikao hicho kwa takriban dakika kumi ili kutafakari suala hilo, hatimae aliwataka wadaiwa kujibu ombi hilo.
  Kwa mujibu wa upande wa wadai, kuwepo kwa ombi hilo mahakamani hapo ni sehemu ya kesi waliyofungua kabla, ambalo limekuja baada ya ukiukwaji wa amri ya mahakama ya kuwazuia viongozi wa ZFA kukanyaga ofisi.
  Viongozi hao pia wamezuiwa kujishughulisha na mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya pamoja na kupiga marufuku shughuli zozote za ZFA ikiwemo uchaguzi.
  Mapema, wakiwa mahakamani hapo, upande wa wadaiwa ulioongozwa na Mwanasheria wa serikali Juma Msafiri Karibona kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali, ulidai umeshindwa kujibu hati ya madai pamoja na ya kiapo kama walivyotakiwa katika kikao kilichopita, kutokana na kutopata taarifa kutoka mamlaka husika.
  Kwa hivyo uliomba muda wa ziada wa kufanya utaratibu wa kupata taarifa hizo ili waweze kujibu hati hiyo ya madai pamoja na ya kiapo.
  Ombi hilo limepingwa na Wakili wa wadai Rajab Abdalla kutoka Kampuni ya AJM Soliciter & Advocate Chamber yenye ofisi zake Amani Wilaya ya Mjini Unguja.
  Katika pingamizi hizo, Wakili huyo alidai huo ni ukiukwaji wa sheria ambazo zinalindwa na mahakama, na ni dhahiri wamekubaliana na wadai kuwa zisifanyike shughuli zozote ndani ya ZFA, na kuiomba mahakama itoe amri zake kwa mujibu wa sheria.
  Hata hivyo baada ya vuta nikuvute hiyo, mahakama imetoa tahafifu kwa wadaiwa na kuwataka kujibu hati ya kiapo, ya madai pamoja na ombi la kudharau mahakama na kuziwasilisha mahakamani hapo kabla ya Januari 28 mwaka huu.
  Tarehe hiyo ndiyo iliyopangwa kwa shauri hilo kusikilizwa tena mahakamani hapo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ZFA WABURUZANA MAHAKAMANI TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top