• HABARI MPYA

  Wednesday, January 21, 2015

  STRAIKA WA KAGERA ASEMA; “AZAM FC BAHATI YAO”

  Na Peter Andrew, MWANZA
  MSHAMBULIAJI wa Kagera Sugar, Atupele Green amesema kwamba bahati haikuwa yao jana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC wakilala 3-1 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana baada ya mechi, Green (pichani kushoto) amesema kwamba amesikitishwa jana timu yake kupoteza mchezo wa pili mfululizo katika Uwanja wa kuhamia, Kirumba, Mwanza.
  Kagera imehamia Mwanza kutokana na Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ambao upo katika ukarabati kwa sasa na tayari imepoteza mechi zote mbili ilizocheza hapo, awali 1-0 dhidi ya Mbeya City mwishoni mwa wiki.
  Katika mchezo wa jana, Kagera Sugar walipoteza nafasi zaidi ya mbili za wazi za kufunga mabao na Green amesema; “Haikuwa bahati yetu. Tulitengeneza nafasi nzuri za kufunga, lakini tulikosa mabao kama mawili hivi,”.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC amesema katika soka unapopoteza nafasi mbili za wazi za kufunga ni jambo baya na haikuwa ajabu wakapoteza mchezo huo.
  “Azam FC walikuwa wana bahati, mipango ilitimia. Walitumia nafasi walizotengeneza na nzuri zaidi waliokoa mabao ambayo wangeweza kufungwa, tunawapongeza kwa ushindi na sisi tunarudi kambini kwenda kufanyia kazi mapungufu,”amesema.
  Pamoja na hayo, Green aliyechezea Coastal Union misimu iliyopita amesema kwamba wana matumaini ya kuzinduka katika mchezo wao ujao, dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara mjini Mwanza tena.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: STRAIKA WA KAGERA ASEMA; “AZAM FC BAHATI YAO” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top