• HABARI MPYA

  Monday, January 05, 2015

  WIMBO WAKO USIPOPENDWA NA WATOTO NA WANAWAKE UJUE IMEKULA KWAKO

  Hadi leo hii bado kuna wasanii wanadhani wimbo bora ni ule wenye njia ngumu za uimbaji, njia zilizojaa ufundi wa hali ya juu, wimbo wenye hadithi ndefu mithili ya “Mario” wa hayati Franco.
  Wanadhani wimbo bora ni ule unaokuwa mgumu kuigika, wako wanaofikiri wimbo unapaswa kuwa kama saini ya benki – mtu asifoji kirahisi.
  Maisha ya sasa yamekuwa ya mwendo kasi, hakuna tena mtu mwenye muda wa kukaa na kujifunza wimbo wako, zile enzi za mshabiki kuchuka kalamu na daftari aanze kuandika mashairi ya wimbo wako ili baadae asome na kuweza kukariri mashairi haupo tena.

  Kama wewe ni msanii mwenye fikra za kutaka mshabiki aende ‘twisheni’ ili akajifunze wimbo wako, basi sanaa yako inaelekea ‘mochwari’.
  Hebu rudini kidogo kwenye wimbo “Jojina” ulioimbwa na marehemu Marijan Rajab kupitia bendi ya Safari Trippers zaidi ya miaka 30 iliyopita.
  Wimbo huo hadi leo, popote pale unapopigwa, asilimia 80 ya watu watainuka kwenye viti vyao kwenda kuucheza huku wakiuimba neno kwa neno, cha kuvutia zaidi ni kwamba katika kundi hilo utawaona pia watu ambao pengine wamezaliwa miaka 10 au zaidi baada ya wimbo huo kurekodiwa.
  Hakuna bendi ya ‘copy’ isiyoupiga wimbo huu, hakuna msanii asiyeweza kuuimba wimbo huu, mara kadhaa utaona mshabiki anakwenda jukwaani na kuachiwa kipaza sauti kisha akauimba “Jojina” kwa ufasaha.
  Nini siri ya “Jojina” kuwa maarufu mithili ya wimbo wa taifa? Jibu ni kwamba huu ni wimbo mwepesi kuuelewa, hauna njia ngumu za uimbaji, hadithi yake ni fupi, upigaji wa vyombo ni wa kawaida sio “mkomoeni”.
  Ukichukua wimbo kama “Mapenzi Yanumiza” wa Twanga Pepeta, unaweza kupata nyimbo hata tatu za staili ya “Jojina”.
  Amini usiamini, mashabiki wa kwanza kabisa wa muziki ni watoto wadogo, kisha dada zetu halafu ndiyo yanafuata makundi mengine.
  Ukitengeneza wimbo ambao mtoto mdogo hawezi kuukariri, hawezi kuuimba basi andika maumivu …ukiona wimbo wako haujawakuna kina dada basi umiza kichwa rudi tena studio.
  Lakini pia kuna kitu kinaitwa mtego, ni lazima wimbo wako uwe na mtego ambao utawanasa watu, imba utakavyoimba, piga utakavyopiga, lakini lazima kuwe na sehemu fulani ya wimbo wako ambayo itawatia wazimu mashabiki wako.
  Kwa bahati mbaya sana, muziki wa dansi ndio muathirika mkubwa wa jambo hili, bendi zetu zinatengeneza nyimbo ngumu, hazina mtego, hadithi ngumu tena zisizonyooka, upigaji wa vyombo wenye kona nyingi kama daraja la mto wami.
  Eti kama bendi ina waimbaji 9 basi angalau waimbaji saba lazima waimbe wimbo mmoja, kila mmoja atatupia mstari wake, mwisho wa siku ukiunganisha wimbo mzima unagundua kuna zaidi ya nyimbo tatu katika wimbo mmoja – wimbo hauleweki. Kuna wakati mwingine ubeti mzima wa mwimbaji hauna ujumbe wowote zaidi ya kujaza majina ya watu mwanzo hadi mwisho.
  Ni kweli kabisa media zimeutupa muziki wa dansi lakini kuna mambo mengine yanachangiwa na wanamuziki wa dansi wenyewe, badilikeni, hakuna ubishi kuwa nyie ni wasanii bora zaidi miongoni mwa aina zote za muziki ila mnajisahau.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WIMBO WAKO USIPOPENDWA NA WATOTO NA WANAWAKE UJUE IMEKULA KWAKO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top