• HABARI MPYA

  Monday, January 12, 2015

  UNAMPONGEZA MFALME MZEE YUSSUF KWA KIPI?

  HIVI karibuni nimemsoma mchambuzi mmoja wa soka wa England akitaka Wayne Rooney atunukiwe tuzo ya mchezaji bora wa msimu nchini humo.
  Lakini mchambuzi huyo hakuishia kusema hivyo tu bali aliainisha na sababu zake kadhaa, mojawapo ni kuwa Rooney atastahili kupewa tuzo hiyo iwapo atafanikiwa japo kuisaidia Manchester United kushika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu ya England.
  Japo ni utashi wake, lakini nilipenda namna mchambuzi huyo alivyolisherehesha wazo lake kwa sababu zenye nyama, ndivyo inavyotakiwa siku zote, ukipendekeza jambo basi shurti uainishe vigezo.

  Hapa nyumbani tumekuwa na matatizo makubwa sana katika kujenga hoja za matukio makubwa ya kiburudani na kimechezo, hoja inakwenda kushoto, tukio linakwenda kulia, hakuna uwiano kabisa.
  Labda nitoe mfano mmoja ambao uko usoni mwetu kuhusu onyesho la swahiba wangu Mfalme Mzee Yussuf pale Travertine Hotel, jijini Dar es Salaam Januri 18.
  Hili ni onyesho kubwa sana kwa maana ya tangazo lake lilivyo, tangazo linasema mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Utamaduni (Nadhani anamaanisha Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), lakini pia kutakuwa na uwepo wa waheshimiwa wabunge.
  Kwa mujibu wa mwaandaaji wa onyesho hilo, Abbas Chezntemba “Cash Money” ambaye ni mmoja wa mapromota wakubwa hapa nchini, shoo hiyo pia itahudhuriwa na wasanii maarufu wa filamu kama vile JB, Ray, Anti Ezekiel na Wema Sepetu.
  Kama vile haitoshi, kwa upande wa burudani licha ya kundi zima la Jahazi Modern Taarab, pia watakuwepo Bi Mwanahawa Ali, Shakila Said, Msagasumu, Rukia Ramadhan na Profesa Mohamed Elyas.
  Onyeshesho hilo limepewa jina la Usiku wa Kihistoria wa kumpongeza Mfalme Mzee Yussuf na ni hapo tu ninapoona mapungufu kwenye onyesho hilo, naona kama kichwa cha habari hakijavishwa nguo - najiuliza kama kusema tu usiku wa kumpongeza Mzee Yussuf inatosha?
  Je, Mzee Yussuf anapongezwa kwa kipi? Tuzo za Kili Music? Uimbaji? Upigaji Kinanda? Kumiliki bendi? Kutangaza kwake nia ya kugombea ubunge au kitu gani hasa?
  Siyo siri kuwa Mzee Yussuf ni msanii wa taarabu mwenye mafanikio makubwa yaliyotokana na muziki wa taarab pengine kuliko msanii yeyote yule.
  Mzee Yussuf anakuwa msanii wa kwanza hapa nchini kumiliki bendi iliyodumu kwa miaka minane mfululizo ikiwa na maonyesho ya kila wiki (ya kiingilio - sio kiingilio kinywaji chako) ambayo hayawahi kusitishwa hata mara moja (ukiondoa mapumziko ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan).
  Tangu kianzishwe kipengele cha mwimbaji bora wa kiume wa taarab kwenye Kili Music Awards, Mzee Yussuf hajawahi kukosa tuzo hiyo. Sasa anaingia mwaka wa kumi tangu aanze kuimba taarab na yuko katika mwaka wa 20 tangu aanze kupiga taarab ya jukwaani.
  Je, sifa zote hizi hakuna hata moja iliyopaswa kuwa kichwa cha habari cha onyesho hilo ili kufanya tukio hilo liwe na sura iliyokamilika? 
  Je Wazari wa Elimu (kama kweli atakuwepo) pamoja na Wabunge (kama nao pia watakuwepo) wanajua wanakwenda Travertine Hotel kumpongeza Mzee Yussuf kwa kipi? Bila shaka hii kitu haijakaa sawa kivile.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: UNAMPONGEZA MFALME MZEE YUSSUF KWA KIPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top