• HABARI MPYA

  Monday, January 12, 2015

  KOPUNOVIC ASEMA MTIBWA SUGAR WAGUMU, LAKINI LAZIMA WAKAE KESHO

  Na Princess Asia, ZANZIBAR
  KOCHA wa Simba SC, Mserbia Goran Kopunovic amesema kwamba Mtibwa Sugar ni timu nzuri, lakini wanajipanga kuhakikisha wanaifunga katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi kesho Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY mjini hapa jana, Kopunovic amesema kwamba anatambua watakutana na timu ngumu katika Fainali, lakini watahakikisha wanatimiza malengo ya kutwaa Kombe.
  “Mtibwa ni timu nzuri, na tulikutana nao katika mechi ya kwanza (Kundi C) wakatufunga, tutaingia katika Fainali kwa lengo la kulipa kisasi na kutwaa Kombe,”amesema. 
  Mserbia huyo aliyeanza kazi Simba SC Januari 2, mwaka huu, amejipongeza kwa kazi nzuri ambayo imeleta mabadiliko katika kikosi cha timu hiyo.
  Kocha wa Simba SC, Goran Kopunovic (kushoto) akiwa na Msaidizi wake, Suleiman Matola

  “Simba sasa inacheza vizuri, timu imebadilika kidogo, wanamiliki mpira na wanajua kuzuia kwa pamoja, nataka hiyo iendelee,”amesema.
  Amefurahi kuongezeka kwa wachezaji wawili ambao walikuwa wana dharula, kipa Ivo Mapunda na mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi na amesema atawatazama mazoezini.
  Kopunovic alianza kazi wakati Ivo na Okwi wana dharula na ruhusa maalum ya uongozi kushughulikia matatizo ya kifamilia na wawili hao waliungana na timu mwishoni mwa wiki.
  Walikuwa benchi wakati Simba SC inashinda 1-0 dhidi ya Polisi katika Nusu Fainali ya michuano hiyo Jumamosi.
  Jana wachezaji wa Simba SC walipewa mapumziko baada ya kazi ngumu na nzuri Jumamosi- na leo wanatarajiwa kuendelea na mazoezi kwa ajili ya Fainali kesho.
  Kikosi cha Simba SC kitamenyana na Mtibwa Sugar katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi kesho Uwanja wa Amaan, Zanzibar

  Kesho itakuwa ni mara ya pili Simba SC kukutana na Mtibwa Sugar katika Fainali ya mashindano haya, baada ya awali kukutana mwaka 2008 na Wekundu wa Msimbazi wakaibuka vinara.   
  Simba SC imewahi kutwaa Kombe la Mapinduzi mara mbili, mwaka 2008 wakiifunga Mtibwa katika Fainali na 2011 wakiifunga Yanga, wakati mara mbili walifungwa katika Fainali, kwanza na Azam FC 2012 na baadaye mwaka jana na KCCA ya Uganda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOPUNOVIC ASEMA MTIBWA SUGAR WAGUMU, LAKINI LAZIMA WAKAE KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top