• HABARI MPYA

  Thursday, January 01, 2015

  TP MAZEMBE KUIPA MAKALI AZAM FC KABLA YA KUIVAA MERREIKH

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC watasafiri kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baadaye mwezi huu kucheza mechi tatu za kujipima nguvu.
  Azam FC imepangwa kuanza na timu tishio katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, El Merreikh ya Sudan na imepanga kwenda kukusanya makali dhidi ya timu bora.
  Azam FC inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kati ya Januari 28 na Februari 3 kwenda Lubumbashi, DRC ambako itacheza na TP Mazembe, Don Bosco na Zesco United ya Zambia.
  Kikosi cha Azam FC leo asubuhi kimeondoka Dar es Salaam kwenda visiwani Zanzibar tayari kucheza michuano ya Kombe la Mapinduzi 2015. 
  Mshambuliaji Mbwana Samatta kwa pamoja na Mtanzania mwenzake, Thomas Ulimwengu ni tegemeo la TP Mazembe

  Azam FC imepangwa Kundi B pamoja na mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda, KMKM na Mtende Rangers zote za Zanzibar, wakati kundi A linajumuisha timu za Yanga SC ya Dar es Salaam, Taifa Jang’ombe, Polisi na Shaba zote za Zanzibar, wakati Kundi C kuna Simba SC, Mtibwa Sugar za Bara, JKU na Mafunzo za Visiwani.
  Michuano hiyo inaanza leo, kwa mchezo baina ya mabingwa wa zamani wa michuano hiyo, Simba SC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Amaan, kuanzia saa 2:15, ambao utatanguliwa na mechi kati ya maafande wa Mafunzo na JKU utakaoanza saa 9:00 mchana.
  Azam FC wao watashuka dimbani kesho kumenyana na mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda kuanzia Saa 11:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa na mechi kati ya KMKM na Mtende Saa 9:00 Alasiri.
  Baadaye usiku, Saa 2:15, Yanga SC watamenyana na Taifa ya Jang’ombe hapo hapo Uwanja wa Taifa, kukamilisha mechi za mzunzuko wa kwanza wa michuano hiyo hatua ya makundi. 
  Timu mbili za kwanza kutoka kila kundi zitafuzu hatua ya robo fainali, na timu mbili zitapatikana kutokana na washindwa waliofanya vizuri (Best Loosers). Fainali ya ngarambe hizo imepangwa kupigwa Januari 13, 2015.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TP MAZEMBE KUIPA MAKALI AZAM FC KABLA YA KUIVAA MERREIKH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top