• HABARI MPYA

  Wednesday, January 21, 2015

  TATIZO NI MAREFA WETU, TIMU ZA JESHI TUNAZICHARUKIA BURE

  ILIKUWA vigumu kuamini kama dakika 90 za mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga SC na Ruvu Shooting zilimalizika bila kadi nyekundu.
  Kwa wastani wa chini kabisa, wachezaji wawili wangeondoka uwanjani mapema kipindi cha kwanza, japo mmoja wa kila timu kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyokithiri.
  Washambuliaji wa Yanga SC wakati wa kona walikuwa hawafikirii namna gani wataingiza mpira nyavuni, badala yake walifikiria jinsi ya kupambana na mabeki wa Ruvu.
  Hamaki ilikuwa kubwa tangu mwanzoni, washambuliaji wa Yanga SC hawakutaka kushindana kwa mpira na mabeki wa Ruvu, bali kwa ubabe.

  Mabeki wa Ruvu walifanikiwa mapema kuziteka akili za washambuliaji wa Yanga SC, ikawa mechi ya kukabana makoo, kupigana viwiko, ngwala na kila aina ya undava.
  Haikuwa ajabu Yanga SC walikosa mabao ya wazi ‘kiajabu ajabu’, kwa sababu akili ya washambuliaji wao siku hiyo, Amisi Tambwe na Kpah Sherman haikuwa kwenye kufunga, bali kuonyeshana ubabe na mabeki wa Ruvu.
  Yule Didier Drogba na mwili wake wote mkubwa, nguvu alizonazo kutokana na lishe ya maana na mazoezi mengi, lakini anapokutana na mabeki hujifanya mlaini.
  Akiguswa kidogo, kajiangusha hadi wakati fulani akawa kero kwa mashabiki wa timu pinzani. Yale yote maarifa. Lakini washambuliaji wa Yanga SC walikua wanapigwa, ngumi, ngwala, viwiko wanagangamala na kujipanga kulipiza.
  Haikuwa mechi ambayo ilistahili kuitwa rasmi na ya mashindano kama Ligi Kuu. Ilikuwa mechi ya kihuni na uhuni uhuni mwingi.
  Ndiyo maana gumzo kubwa baada ya mchezo huo, ukiacha washambuliaji wa Yanga SC kukosa mabao mengi ya wazi, ilikuwa ni namna wachezaji walivyotambiana kwa ubabe.
  Washambuliaji wa Yanga SC walidhihirisha maarifa yao haba na ukomavu mdogo wa kisoka siku hiyo- ndiyo maana wakaufanya mchezo mwepesi uwe mgumu zaidi.
  Mchezo uliopita wa Ligi Kuu kuzikutansisha Yanga na Ruvu ulikuwa msimu ulipota na timu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), ilipigwa mabao saba.
  Kwa sababu wakati ule, safu ya ushambuliaji ya Yanga SC ilikuwa ina watu wenye maarifa ya kisoka, bahati mbaya wengi hawapo tena. Nawazungumzia Waganda Hamisi Kiiza, Emmanuel Okwi na Mrundi Didier Kavumbangu pamoja na wazalendo Mrisho Ngassa na Simon Msuva.
  Ngassa kwa sasa kama anaondoka hivi kwenye kikosi cha kwanza Yanga SC, wakati Msuva alikuwepo na alikosa mabao kibao ya wazi.
  Lakini watu wanasema, mtu huiga tabia za watu anaokuwa nao, Msuva naye eti siku ile alikuwa anacheza kindava. Mbrazil Andrey Coutinho naye kadhalika.
  Mashabiki na baadhi ya vyombo vya habari wamelalamika vitendo ambavyo si vya kiuanamichezo vilivyokuwa vinafanywa na mabeki wa Ruvu na wakafika mbali wakitaka timu za majeshi ziwe na Ligi yao.
  Kuna mambo mawili, timu za jeshi na sheria 17 za mchezo. Hakuna sheria maalum wala marefa maalum kwa ajili ya mechi zinazohusu timu za majeshi. 
  Hata Polisi Moro ni timu ya jeshi, JKT Ruvu pia, au Prisons- lakini hawa hawachezji kindava. Pale Ruvu Shooting kuna beki anaitwa George Michael, anasifiwa muda mrefu kwa mchezo ule, naye anavimba kichwa anaona anafanya sawa.
  Bahati mbaya marefa, wameshindwa kumbadilisha. Rahisi tu kumbadilisha, anafanya kitu, anapewa kadi nyekundu. Anaiachia timu pungufu, ikifungwa kocha wake, Thoma Olaba atauona umuhimu wake.
  Lakini beki yule Jumamosi kawatandika wachezaji wa Yanga kwa staili zote na bado hakupewa kadi stahili. Mbaya zaidi, wachezaji wa Yanga nao wakaingia kwenye mtego wa kulipiziana na kuifanya mechi iwe ya ovyo.
  Yanga SC wataongea sana kwa hasira za sare na kulaani timu za majeshi, lakini hilo si tatizo kwa sasa. Ligi yetu inazihitaji hizo timu za heshi kutokana na hali halisi ya kiuchumi ya klabu zetu za mtaani.
  Timu za majeshi zina uwezo wa kutunza wachezaji ambao kesho wanakuwa tegemeo la taifa na hata kusajiliwa na hizo hizo timu za wananchi.
  Frank Domayo aliingia Yanga akitokea wapi? Au yule Edward Charles, au Hassan Dilunga. Sasa bila timu za Majeshi, Yanga wangewapataje nyota hao?
  Hapa tuzungumzie udhaifu wa marefa wetu na kufikiria namna ya kuifanya Ligi yetu, iwe na marefa bora na waadilifu. Hilo ndilo la msingi.
  Lakini pia, na makocha wa Yanga SC wawafundishe wachezaji wao maarifa ya kisoka, wasije wakarudia makosa waliyofanya Jumamosi.
  Pongezi kwa kazi nzuri ya vyombo vya habari kutoa picha zinazoonyesha matukio ya kihuni katika mchezo wa Yanga na Ruvu, kinachofuata ni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchukua hatua. Tatizo marefa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TATIZO NI MAREFA WETU, TIMU ZA JESHI TUNAZICHARUKIA BURE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top