• HABARI MPYA

  Wednesday, January 21, 2015

  NOOIJ: WACHEZAJI WA SIMBA, YANGA NA AZAM NDIYO WANAFAA KWA TIMU ZA TAIFA

  Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
  KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mart Nooij amesema anahitaji wachezaji wadogo, lakini wenye uzoefu kuwandaa kwa ajili za mechi za kufuzu CHAN, baadaye mwaka huu.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika ukumbi wa mikutano, Mwanza Hotel mjini hapa, Mholanzi huyo amesema kwamba ni kwa sababu hiyo amechukua wachezaji wengi wa timu kubwa katika kikosi chake kitakachomenyana na Rwanda kesho.
  Timu ya taifa chini ya umri wa miaka 23, maarufu kama Taifa Stars Maboresho kesho itamenyana na Rwanda katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.  
  Kocha Mart Nooij (kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari leo Mwanza Hotel
  Manahodha wa timu hiyo, Said Ndemla kushoto na Simon Msuva kulia wakizungumza na Waandishi wa Habari
  Wachezaji wa Taifa Stars Maboresho wakipata mlo wa mchana Mwanza Hotel

  Na kocha Nooij, anayesaidiwa na mzalendo Salum Mayanga, ameita vijana 22, zaidi kutoka klabu za Yanga SC, Azam FC na Simba SC kwa sababu anaamini wana uzoefu. 
  “Klabu kama Kagera Sugar na Stand United, hazichezi mashindano ya kimataifa, zinaweza kuwa na vijana wenye vipaji, lakini hawana uzoefu. Kama tunataka kufanya vizuri katika CHAN ili tufuzu, tunahitaji wachezaji wazoefu na damu changa,”amesema.
  Wachezaji walioitwa na kocha huyo ni Peter Manyika, Benedicto Tinoco, Miraj Adam, Gardiel Michael, Joram Mgeveke, Andrew Vincent, Edward Charles, Salum Telela, Abdu Banda, Said Juma ‘Kizota’, Said Ndemla na Abubakar Ali.
  Wengine ni Hassan Dilunga, Shiza Ramadhani, Kevin Firday, Simon Msuva, Salum Mbonde, Rashid Mandawa, Adam Paul, Alfred Juma, Mohammed Hussein na Hussein Moshi.
  “Tuna timu nne za taifa, tuna U17, U20, U23 ambayo ni Olimpiki na tuna Taifa Stars. Katika timu hii tumechukua wachezaji chini ya umri wa miaka 22, huwezi kuona Nadir Haroub, Mbwana Samatta wala Mrisho Ngassa hapa,”.
  “Tunataka kutengeneza haraka kikosi cha CHAN, tunahitaji vijana wadogo na wazoefu, tumekuja na vijana hawa Mwanza ili waonyeshe uwezo wao. Miaka 20 kijana tayari anacheza klabu kubwa Tanzania na ni mchezaji wa Tanzania mwenye uzoefu,”amesema.
  Nooij ameonyesha imani yake kwa vijana hao, akisema kwamba baada ya mafundisho ya soka, sasa wanatakiwa kuonyesha uwezo wao dhidi ya Rwanda kesho.
  “Vijana wetu tumewachukua tumewapeleka kuwafundisha kuogelea, sasa wamejua kuogelea, wanatakiwa kutuonyesha wanajua kuogelea,”alisema Nooij akimaanisha anataka vijana hao waonyeshe uwezo wao dhidi ya Amavubi kesho.
  Rwanda inatua leo mjini Mwanza ikiwa na kikosi kamili cha timu ya taifa ya kwanza ya nchi hiyo, chini ya Nahodha, Haruna Niyonzima anayechezea Yanga SC ya Tanzania kwa ajili ya mchezo wa kesho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NOOIJ: WACHEZAJI WA SIMBA, YANGA NA AZAM NDIYO WANAFAA KWA TIMU ZA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top