• HABARI MPYA

  Tuesday, January 13, 2015

  SIMBA BINGWA KOMBE LA MAPINDUZI 2015

  SIMBA SC wametwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2015 baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Shujaa wa Simba SC alikuwa ni kipa Ivo Mapunda aliyetokea benchi dakika ya 90 kwenda kuchukua nafasi ya Peter Manyika na kuokoa penalti ya mwisho ya Mtibwa iliyopigwa na Vincent Barnabas.
  Awali, Ivo alishuhudia penalti ya Ibrahim Rajab ‘Jeba' ikigonga mwamba wa juu wakati upande wa Simba SC, penalti ya Shaaban Kisiga ‘Malone’ ilipanguliwa na kipa wa Mtibwa, Said Mohammed Kasarama.
  Wachezaji wa Simba SC wakiwa wamembeba kipa wao, Ivo Mapunda baada ya kupangua penalti ya mwisho ya Mtibwa Sugar iliyopigwa na Vincent Barnabas na kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Mapinduzi usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar
  Penalti za Simba SC zilifungwa na Awadh Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Dan Sserunkuma, wakati za Mtibwa zilifungwa na Aly Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhani Kichuya.
  Kipa wa Mtibwa ndiye ametajwa kipa bora wa mashindano, baada ya kufungwa bao moja katika mechi tano, mchezaji bora beki Salim Mbonde wa Mtibwa na mfungaji bora Simon Msuva wa Yanga SC, mabao manne.

  Katika mchezo huo, timu zote zilishambuliana kwa zamu ndani ya dakika 90 na sifa ziwaendee makipa wote, Peter Manyika wa Simba na Said Mohammed wa Simba kwa kuokoa michomo kadhaa langoni mwao.  
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika/Ivo Mapunda dk90, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi, Said Ndemla/Shaaban Kisiga ‘Malone’ dk89, Ibrahim Hajibu/Elias Maguri dk65, Dan Sserunkuma na Emmanuel Okwi/Awadh Juma dk75.
  Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Ally Lundenga, David Luhende, Salim Mbonde, Andrew Vincent, Shaaban Nditi, Mussa Nampaka/Ibrahim Rajab ‘Jeba’ dk66, Muzamil Yassin, Ame Ally/Abdallah Juma dk90, Ally Shomary/Ramadhani Kichuya dk87 na Mussa Hassan ‘Mgosi’/Vincent Barnabas dk78.
  Kikosi cha Simba SC kilichoanza katika mchezo wa leo
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA BINGWA KOMBE LA MAPINDUZI 2015 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top