• HABARI MPYA

  Sunday, January 04, 2015

  SIIONI AZAM FC YA KUFURUKUTA MBELE YA EL MERREIKH

  MWEZI ujao, Azam FC na Yanga SC zitaanza kucheza michuano ya Afrika, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa.
  Mabingwa wa Tanzania, Azam FC watamenyana na El Merreikh ya Sudan katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Februari 13 na 15 wakati marudiano yatakuwa Februari 27 na Machi 1 na Azam FC wataanzia nyumbani.
  Wakifanikiwa kuwatoa Wasudan hao, Azam FC watamenyana na mshindi kati ya Lydia Ludic B.A ya Burundi na Kabuscorp do Palanca ya Angola
  Katika Kombe la Shirikisho, Yanga SC itamenyana na BDF IX ya Botswana katika hatua ya awali, mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Februari 13 na 15 wakati marudiano kati ya Februari 27 na Machi 1, Yanga SC nao wakianzia nyumbani.

  Wakifanikiwa kuvuka mtihani huo, Yanga watamenyana na mshindi kati ya Sofapaka ya Kenya Platinum ya Zimbabwe.
  Timu hizo mbili, wiki iliyopita zilikutana katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania mzunguko wa kwanza na kutoka sare ya 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Baada ya hapo, zimehamia Zanzibar ambako zinashiriki michuano ya wiki mbili, Kombe la Mapinduzi, inayoshirkisha timu za Bara, Visiwani na moja ya Uganda, KCCA ambao ndiyo mabingwa watetezi wa Kombe hilo.
  Tayari kila timu imecheza mechi moja hadi sasa, Yanga SC ikishinda 4-0 dhidi ya timu ya Daraja la Pili Zanzibar, Taifa Jang’ombe na Azam FC wakitoa sare ya 2-2 na KCCA.
  Azam walicheza na mpinzani mgumu, lakini bado matokeo na kiwango walichoonyesha kwenye mchezo huo si cha kuridhisha, ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa michuano ya Afrika.
  Ningependa kuizungumzia Azam FC tu leo, ingawa Yanga SC nao wakiwa ndiyo kwanza wamemrejesha kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm tunampa muda, kwani huko nako mambo bado.
  Pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanywa ndani ya Azam FC kwa kusajili wachezaji bora kila idara, bado timu hiyo haichezi soka ya kiwango cha Ligi ya Mabingwa.
  Wachezaji wako fiti, ndiyo. Wanamudu dakika 90, wana kasi uwanjani, nguvu na kwa ujumla wana uwezo, lakini kwa maana ya uchezaji mzuri kama timu, Azam FC bado.
  Mwishoni mwa mwaka, Azam FC walimuongezea nguvu kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog kwa kumuajiri aliyekuwa kocha wa KCCA, Mganda George ‘Best’ Nsimbe.
  Nsimbe alikuja baada ya kujiuzulu kwa kocha Muingereza, Kali Ongala aliyekuwa Msaidizi tangu enzi za Muingereza mwenzake, Stewart John Hall.
  Matarajio ni kwamba, baada ya kuongezwa kocha mzoefu, George Best na kusajiliwa kwa wachezaji wengine bora kama beki kutoka Ivory Coast, Serge Wawa Pascal aliyekuwa anachezea El Merreikh ya Sudan, Amri Kiemba kutoka Simba SC kwa mkopo na Brian Majwega kutoka KCCA ya Uganda, mambo yangebadilika Azam FC.  
  Lakini ukweli ni kwamba Azam FC haichezi kwa kiwango cha kutia matumaini kama inaweza kuvuka japo raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Tunaifahamu Merreikh, ni timu bora na ina wachezaji bora, akiwemo mshambuliaji wa Mali, Mohammed Traore ambaye Azam FC walitaka kumsajili, lakini hawakufanikiwa.
  Unapopangiwa kucheza na timu ya aina ya Merreikh, lazima uwe na timu bora, lakini si hii Azam FC ya sasa tunayoiona, ukaitarajia itaitoa Merreikh. Itokee bahati sana.
  Desturi ya kupeana ‘sifa za kinafiki’ ili kufurahishana na kuwapendezesha mashabiki, au kutaka kuvutia wasomaji na watazamaji ndiyo kwa kiasi kikubwa imechangia udhaifu wa timu zetu. 
  Ukishaandika; “Azam noma, Yanga SC tisha mbaya, Simba SC ni hatari”- basi hata wahusika katika timu hizo wanaamini wako vizuri tu, mwisho wa siku yanawadia mashindano ya Afrika tunaendelea kudhalilika.
  Ndiyo maana, miaka inakatika Tanzania haina cha kujivunia kwenye michuano ya Afrika zaidi ya Simba SC kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa mwaka 1974 na Fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993.
  Zaidi ya hapo, baada ya kuanza kwa mfumo mpya wa michuano ya Afrika, timu mbili tu zilifika hatua ya makundi, kwanza Yanga SC mwaka 1998 na baadaye Simba SC 2003.
  Kama unatoa sare nyumbani na KCCA ya Uganda, unawezaje kutarajia kuifunga Merreikh hata mechi ichezwe Chamazi?
  Katika wiki ya kwanza ya Januari, nawaambia Azam FC kwamba wana kazi ya kufanya kwa siku chache zilizobaki kabla ya kukutana na El Merreikh. Kwa sababu hivi sasa, siioni Azam FC ya kufurukuta mbele ya Wasudan hao, ambao wanapoingia kwenye michuano hiyo lengo la kwanza ni kufika hatua ya makundi. Heri ya mwaka mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIIONI AZAM FC YA KUFURUKUTA MBELE YA EL MERREIKH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top