• HABARI MPYA

  Sunday, January 18, 2015

  PLUIJM, MKWASA KAZI WANAYO YANGA SC!

  KATIKA mechi tatu mfululizo zilizopita, Yanga SC imeonyesha udhaifu mkubwa katika safu yake ya ushambuliaji, kutokana na kukosa mabao mengi ya wazi.
  Yanga SC ilishinda 1-0 kwa mbinde katika mechi na Shaba Kombe la Mapinduzi, siku ambayo washambuliaji wake walikosa mabao zaidi ya matano ya wazi.
  Ikafungwa 1-0 na JKU katika michuano hiyo, siku nyingine tena washambuliaji wake wakikosa mabao zaidi ya matano ya wazi.
  Baada ya kutolewa katika Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi, kocha Mholanzi Hans van der Pluijm aliyerejea kazini Desemba mwishoni kumpokea Mbrazil, Marcio Maximo akasema anakwenda kufanyia kazi tatizo hilo.

  Yanga SC ikawa kambini kwa wiki Bagamoyo ikijifua kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani.
  Mchezo huo ulifanyika jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwa mara nyingine, washambuliaji wa Yanga SC walikosa mabao matano au zaidi ya wazi katika sare ya 0-0.
  Mtu anakosa bao amebaki yeye na kipa kama anapiga penalti- huyo ni Simon Msuva, lakini pia mipira mingi ya kutokea pembeni washambuliaji wa Yanga hawaipati.  
  Yanga SC kwa sasa inacheza vizuri, inajua kupangilia mashambulizi, lakini tatizo ni kufunga mabao- wanakosa mengi ya wazi.
  Jana ilibaki kidogo wapate ‘bakhshishi’ ya kukosa mabao ya wazi kwa kufungwa wao, kama si jitihada za beki Rajab Zahir kuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni dakika za lala salama.
  Siku wanatolewa na JKU katika Kombe la Mapinduzi, pia walikosa mabao mengi ya wazi, lakini kosa moja walilofanya, wapinzani wakatumia vizuri nafasi hiyo kupata bao la ushindi.
  Baada ya Kombe la Mapinduzi, Pluijm alisema anakwenda kufanyia kazi tatizo hilo, lakini wiki moja baadaye imerudi Yanga ile ile ya kukosa kosa mabao.
  Na huwezi kusema Yanga SC ina washambuliaji butu, hapana- wote Amisi Tambwe, Kpah Sherman na Msuva wana rekodi nzuri za kufunga mabao huko nyuma sawa tu na Dan Mrwanda, Hussein Javu, Mrisho Ngassa na Jerry Tegete.
  Lakini kwa sasa, makali yao yamepotea na niliwahi kuandika wiki iliyopita kwamba kutokana na imani haba za wachezaji wetu, itafikia washambuliaji wa Yanga SC watashikana uchawi. Watatuhumiana kulogana.
  Iliwahi kutokea, mwaka juzi mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbangu ambaye kwa sasa amehamia Azam FC aliingia kwenye ugomvi na Tegete akimtuhumu kumloga.
  Siamini uchawi popote, si katika soka tu- sijui labda kwa sababu ya imani yangu au vipi, lakini kwa imani haba za wachezaji wetu kinachofuata ni hicho.
  Ukitazama namna Yanga SC wanavyocheza pale mbele, utagundua kuna tatizo. Mashambulizi yanapangwa vizuri, lakini namna ya kumalizia nafasi ndiyo tatizo.
  Na litaendelea kuwa tatizo, iwapo baada ya mechi kama ya jana katika mazoezi yanayofuata makocha hawatafanyia kazi tatizo hilo.
  Kweli kuna bahati mbaya, lakini inapofikia kwa kiwango cha Yanga SC, wachezaji wote wanakosa mabao, tena ya wazi namba ile, basi kuna tatizo.
  Katika mechi mbili zilizopita, wachezaji Andrey Coutinho na Simon Msuva wanaonekana kabisa kuchangia kutokana na kusahau majukumu yao kama viungo washambuliaji wanaotakiwa kuwasetia mipira washambuliaji, na kuweka mbele uchu wa kutaka kufunga wenyewe.
  Aina ya mipira wanayoingiza kutokea pembeni si ya kuwalenga washambuliaji wao, bali ni kutaka wafunge wenyewe. Tumeliona hilo katika mechi mbili zilizopita na hatujui itakuwaje katika mechi ijayo.
  Lakini hapa unaizungumzia timu ambayo mwezi ujao itacheza mechi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya BDF ya Botswana.  
  Unaweza kutabiri nini katika safari ya Yanga SC Kombe la Shirikisho ikiwa hali ndiyo hii ya sasa wachezaji wanakosa mabao mengi ya wazi. Ukweli ni kwamba, makocha wa Yanga SC, Pluijm na Msaidizi wake Charles Boniface Mkwasa wana kazi ya kufanya katika kipindi kifupi kilkichobaki kabla ya kuingia kwenye michuano ya Afrika, vinginevyo hadithi itaendelea kuwa ile ile, kutolewa mapema. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM, MKWASA KAZI WANAYO YANGA SC! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top