• HABARI MPYA

  Sunday, January 18, 2015

  PLUIJM AWATOLEA UVIVU WASHAMBULIAJI YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amesema washambuliaji wake waliigharimu timu jana kupoteza pointi mbili dhidi ya Ruvu Shooting.
  Yanga SC jana jioni imelazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku washambuliaji wake wakikosa mabao ya wazi. 
  “Huwezi kusema chochote, wanastahili lawama kwa matokeo haya. Ulikuwa mchezo wa kumalizika ndani ya dakika 45 za kwanza, lakini walishindwa kutumia nafasi nzuri kabisa.
  Makocha wa Yanga SC, Hans van der Pluijm (kushoto) na Charles Boniface Mkwasa

  Hii ni mbaya kama itaendelea, nimefanyia kazi hili wiki yote hii, lakini nasikitika limejirudia tena. Hatujakata tamaa, tunarudi mazoezini kujiandaa na mchezo ujao, na tutafanyia kazi tena hili,”amesema.  
  Washambuliaji wa Yanga SC, Kpah Sherman, Amisi Tambwe, Simon Msuva na Andrey Coutinho wote walikosa mabao ya wazi jana. 
  Winga Simon Msuva ndiye aliyewasikitisha zaidi wana Yanga kwa kupoteza nafasi tatu za wazi za kufunga dakika za 10, 13 na 38 na Mbrazil Andrey Coutinho alipoteza nafasi mbili, huku nyingine ikipotezwa na Amisi Tambwe. 
  Kipindi cha pili, pamoja na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm kubadilisha washambuliaji, akiwatoa Coutinho, Msuva na Tambwe ambao nafasi zao zilichukuliwa na Hussein Javu, Dan Mrwanda na Mrisho Ngassa, lakini bado haikuwa siku ya Yanga SC.
  Na ilibaki kidogo Yanga wapoteze mchezo kama si jitihada za beki Rajab Zahir kuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni kufuatia kipa wake, Ally Mustafa ‘Barthez’ kulambwa chenga na Abdulrahman Mussa dakika ya 81.
  Yanga SC sasa inaelekea kwenye maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Coastal Union katikati ya wiki.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: PLUIJM AWATOLEA UVIVU WASHAMBULIAJI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top