• HABARI MPYA

  Sunday, January 04, 2015

  OWINO HANA RAHA SIMBA SC KISA TAARIFA ZA ‘UMBEYA’

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Simba SC, Joseph Owino anaonekana kuvurugwa na taarifa kwamba hataongezewa Mkataba mwishoni mwa msimu, naye kama ameamua kususa.
  Owino alipewa ruhusa ya kwenda mapumzikoni nyumbani Uganda, baada ya mechi ya Nani Mtani Jembe Desemba 13, lakini baada ya muda wake kumalizika alituma taarifa Dar es Salaam kwamba anaumwa hawezi kurudi kwa sasa.
  Hata hivyo, uongozi wa Simba SC umemuambia beki huyo wa kati anatakiwa kurejea Dar es Salaam atibiwe na klabu, vinginevyo atahesabiwa kama mtoro.
  Uchunguzi uliofanywa na BIN ZUBEIRY umebaini kwamba Owino hana furaha Simba SC kufuatia kuwapo kwa tetesi kwamba, yeye ndiye ataachwa kumpisha mshambuliaji Mkenya, Paul Kiongera aliye majeruhi kwa sasa.
  Nahodha wa Simba SC, Joseph Owino katikati hana furaha kwa sasa na kama ameamua kususa 

  Kiongera anatarajiwa kuwa fiti kabisa hadi kufika Machi mwaka huu na Simba SC imedhamiria kumsajili katika kikosi cha msimu ujao.
  Kwa kuwa kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zinataka wachezaji watano tu wa kigeni, Simba SC italazimika kumkata Mganda mmoja, kati ya Owino, Juuko Murushid, Emmanuel Okwi, Dan Sserunkuma na Simon Sserunkuma ili kumuingiza Kiongera. 
  Wakati huo huo, klabu tatu Azam FC, Yanga na Simba SC zinaendelea kufanya ushawishi idadi ya wachezaji wa kigeni iongezwe kutoka watano hadi saba, ingawa hilo Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amekuwa mstari wa mbele kulipinga.
  Malinzi anaamini kuruhusu wachezaji wa kigeni zaidi kutapunguza thamani ya wachezaji wa nyumbani katika klabu hizo kubwa, ambazo zinategemewa kuzalisha na kulea wachezaji wa timu za taifa.
  Habari za ndani kutoka Simba SC zinasema kwamba suala la nani ataachwa kumpisha Kiongera litaamuliwa na kocha mpya, Mserbia Goran Kopunovic baada ya kuwa na wachezaji wote kwa sehemu iliyobaki kuelekea mwisho wa msimu. 
  Wakati huo huo, wachezaji wengine wawili Waganda wa Simba SC, Simon Sserunkuma na Okwi wanatarajiwa kujiunga na timu kuanzia leo visiwani Zanzibar.
  Simba SC ipo visiwani Zanzibar inacheza michuano ya Kombe la Mapinduzi, ikiwa imepangwa Kundi C pamoja na Mtibwa Sugar, Mafunzo na JKU. Tayari Wekundu hao wa Msimbazi, wamecheza mechi mbili na kufungwa moja 1-0 na Mtibwa na kushinda moja 1-0 na Mafunzo.
  Watakamilisha mechi zao za Kundi C kwa kucheza na JKU kesho Uwanja wa Amaan na wanahitaji ushindi ili kwenda Robo Fainali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OWINO HANA RAHA SIMBA SC KISA TAARIFA ZA ‘UMBEYA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top