• HABARI MPYA

  Sunday, January 04, 2015

  COUTINHO APIGA MBILI, YANGA YAUA TENA 4-0 KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MBRAZIL Andrey Coutinho ameng’ara leo akifunga mabao mawili, Yanga SC ikishinda 4-0 dhidi ya Polisi ya Zanzibar katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Wazi Yanga SC imekwishatinga Robo Fainali ya michuano hiyo baada ya kuwa kileleni mwa kundi hilo, kwa mabao manane na pointi sita baada ya mechi mbili.
  Hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mbrazil Andrey Coutinho na Mliberia Kpah Sherman.
  Coutinho alifunga bao la kwanza dakika ya 27 baada ya kupokea pasi ya beki Oscar Joshua pembezoni mwa Uwanja kushoto na kuwakokota mabeki wawili wa Polisi badi kwenye boksi akafumua shuti kumchambua kipa Nasir Suleiman.
  Andrey Coutinho (kushoto) akipongezana na wenzake, Sherman na Tambwe kulia baada ya kufunga mabao mawili leo Amaan  

  Sherman naye akafunga la pili dakika ya 33 baada ya kudondoshewa pasi ya kichwa Mrundi Amisi Tambwe, kufuatia krosi ya Simon Msuva.
  Kipindi cha pili, Yanga SC iliendelea kung’ara na kufanikiwa kupata bao la tatu mapema dakika ya 56 kupitia kwa Coutinho, aliyepiga shuti la mpira wa adhabu nje ya boksi pembeni kulia, baada ya Amisi Tambwe kuangushwa.
  Bao hilo liliwatia ‘chaji zaidi’ Yanga SC na kuzidi kushambulia langoni mwa Polisi, hasa baada ya kocha Mholanzi Hans van der Pluijm kuingiza nguvu mpya, Mrisho Ngassa, Hassan Dilunga na Danny Mrwanda waliokwenda kuchukua nafasi za Nizar Khalfan, Kpah Sherman na Coutinho.  
  Beki wa Polisi akimchezea rafu Coutinho
  Sherman akimuacha chini beki wa Polisi

  Simon Msuva aliifungia Yanga SC bao la nne dakika ya 80, baada ya kupewa pasi nzuri na Mrisho Khalfan Ngassa.
  Katika mchezo uliotangulia, mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda wamewatandika Mtende 3-0, mabao ya Herman Wasswa dk41, William Wadri dakika ya 65 na 66. 
  Taifa ya Jang’ombe imeilaza 1-0 Shaba Uwanja wa Mao dze Tung, wakati mchezo kati ya Azam FC na KMKM utakamilisha mechi za leo za Kombe la Mapinduzi kuanzia Saa 2:15 usiku Uwanja wa Amaan pia.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Rajab Zahir dk86, Salum Telela/Said Juma ‘Kizota’ dk86, Simon Msuva, Nizar Khalfan/Hassan Dilunga dk46, Kpah Sherman/Mrisho Ngassa dk65, Amisi Tambwe na Andrey Coutinho/Danny Mrwanda dk65.
  Polisi; Nasir Suleiman, Mohammed Seif, Mwita Mohammed, Abdallah Mwalimu, Mohammed Ally, Daniel Justin, Samir Vincent/Steven Emmanuel dk55, Ali Khalid, Said Bakari/Abdallah Omar dk55, Frank Temis na Mohamed Hassan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: COUTINHO APIGA MBILI, YANGA YAUA TENA 4-0 KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top