• HABARI MPYA

  Thursday, January 01, 2015

  MWADUI FC YAENDELEZA MOTO, YAICHAPA PANONI FC 2-1

  Na Philipo Chimi, SHINYANGA
  TIMU ya Mwadui FC ya Kishapu, Shinyanga imeendeleza mbio zake za kuelekea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya jana kuichapa mabao 2-1 Panoni FC ya Moshi katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza.
  Katika mchezo huo, Panoni FC ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji wake, Ayubu Shilyanda katika dakika ya 17, lakini dakika ya 21 Razack Khalfan akaisawazishia Mwadui.
  Kipindi cha pili Mwadui FC walirudi uwanjani kwa nia ya kupata ushindi na wakafanikiwa kutoboa nyavu za Panoni kwa mara ya pili kupitia kwa mchezaji wao matata, Bakari Kigodeko dakika ya 88.
  Mwadui FC inanukia Ligi Kuu

  Mara baada ya mchezo huo, kocha wa Mwadui, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’, alisema ushindi huo ni mafanikio kwao na kwamba dhamira yao siku zote ni ushindi.
  “Sisi ushindi ni kawaida yetu na huu ni mwanzo tu, lazima tuingie Ligi Kuu, lakini niwaombe wapenzi wa mpira wa miguu mkoani Shinyanga waendelee kuzisapoti timu zao za Shinyanga, Stand United pamoja na Mwadui ili tufike mbali,” alisema Kihwelu.
  Sasa Mwadui FC imefikisha pointi 28 katika Kundi A Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, hivyo kuendelea kuwa kileleni, wakifuatiwa na mahasimu wao, Toto African ya Mwanza wenye pointi 23 baada ya jana kutoka sare na JKT Oljoro ya Arusha.
  Panoni inabaki na pointi 15 na Mwadui sasa wanajiandaa kuivaa JKT Oljoro ya Arusha katika mchezo ujao.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWADUI FC YAENDELEZA MOTO, YAICHAPA PANONI FC 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top