• HABARI MPYA

  Thursday, January 01, 2015

  GORAN AMKATAA NTAGWABILA, AMCHAGUA MNYARWANDA MWINGINE AWE MSAIDIZI WAKE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSERBIA Goran Kopunovic amesaini Mkataba wa mwaka mmoja, ambao anaweza kufukuzwa baada ya msimu iwapo hatafanya vizuri.
  Mkataba wa Goran aliosaini leo Dar es Salaam unasema iwapo uongozi utaridhishwa na kazi yake, utampa Mkataba mwingine wa miaka miwili, lakini kama kazi yake haitakuwa na tija, ataondolewa mwishoni mwa msimu, Juni mwakani.
  Lakini Goran naye amekataa Jean Marie Ntagwabila kuwa Msaidizi wake, badala yake amempendekeza Alphonse Gatera aliyekuwa Msaidizi wake wakati anafundisha Polisi ya Rwanda.
  Goran Kopunovic amesaini Mkataba ambao anaweza kufukuzwa mwishoni mwa msimu

  Gatera anatarajiwa kuwasili kesho Dar es Salaam kusaini Mkataba wa kufanya kazi Simba SC, ambayo kwa sasa kikosi chake kipo visiwani Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi.
  Kopunovic baada ya kusaini Mkataba leo, amepanda boti kwenda Zanzibar kuungana na timu, iliyo chini ya Kocha Msaidizi, Suleiman Matola baada ya kufukuzwa kwa Mzambia, Patrick Phiri. Matola atakuwa Msaidizi namba mbili wa Kopunovic.
  Usiku wa leo, Simba SC itamenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Amaan, Zanzibar na bila shaka Mserbia huyo atakuwa jukwaani kuiangalia timu kabla ya kuanza kazi rasmi kesho. 
  Jean Marie Ntagwabila alikuwa tayari kuwa Msaidizi wa Kopunovic Simba SC na akasema kwamba anamfahamu Mserbia huyo kwa sababu walifanya naye kazi Rwanda na anaheshimu uwezo wake.
  Wanaungana tena; Kopunovic kulia akiwa Gatera enzi zao Polisi Rwanda

  Ntagwabila aliifanya APR iwe tishio mno kiasi cha kufikia kuifunga Zamalek ya Misri mabao 4-1 mwaka 2004 katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikitoka kufungwa 3-2 katika mchezo wa kwanza Cairo.
  APR ilisonga mbele hatua ya 16 Bora, ambako ilikwenda kutolewa kwa mbinde na Africa Sports ya Ivory Coast kwa penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
  Simba SC imeachana na Phiri baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu chini yake tangu ameanza kazi Agosti mwaka huu akirithi mikoba ya Zdravko Logarusic raia wa Croatia.
  Simba SC iliachana na Logarusic kwa sababu tu ya tabia zake za kifedhuli, ambazo ilijaribu sana kumkemea, lakini hakuwa tayari kubadilika na ikaamua kumrejesha Phiri kutokana na historia yake ya kufanya kazi kwa mafanikio awali katika klabu hiyo, lakini safari hii mambo hayakuwa kama yalivyotarajiwa.
  Phiri aliiongoza Simba SC kwa mara ya mwisho Desemba 26, ikifungwa 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Tangu amekuja Simba SC kwa mara ya tatu Agosti mwaka huu, Phiri ameiongoza Simba SC katika mechi 22 na kushinda nane, kati ya hizo moja tu ya Ligi Kuu 1-0 dhidi ya Ruvu Shooitng na moja ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga SC 2-0, wakati amefungwa tano na kutoka sare tisa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GORAN AMKATAA NTAGWABILA, AMCHAGUA MNYARWANDA MWINGINE AWE MSAIDIZI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top