• HABARI MPYA

  Wednesday, January 14, 2015

  MTIBWA SUGAR: KUUZA WACHEZAJI SASA BASI, TUNATAKA MATAJI

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MTIBWA Sugar inafikiria kuacha desturi ya kuuza wachezaji wake, ili kuimarisha kikosi kwa ajili ya kushinda mataji.
  Mratibu wa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Jamal Bayser ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba sasa wanafikiria kudumu na wachezaji wao ili wawe na kikosi imara cha kushinda mataji.
  “Watu wengi wanatushauri hivyo na tumeona kuna umuhimu wa kufanya hivyo. Tunataka kushinda mataji sasa,”amesema. 
  Kwa muda sasa, Mtibwa Sugar imekuwa kama chuo cha kuzalisha nyota wanaokwenda kuwika timu nyingine za Ligi Kuu, lakini hali hiyo imekuwa ikiirudisha nyuma timu hiyo katika mbio za ubingwa.  
  Mratibu wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser (kushoto) akifuatilia Fainali jana Kombe la Mapinduzi
  Kikosi cha Mtibwa Sugar kilichopoteza mchezo kwa matuta jana 

  Kwa mara nyingine, msimu huu Mtibwa Sugar inaonekana kuwa na kikosi imara kinachoweza kubeba ubingwa, hadi sasa ikiwa inaongoza Ligi Kuu.
  Lakini tayari nyota wake kadhaa wanamezewa mate na vigogo wa soka nchini, Simba SC, Yanga na Azam FC miongoni mwao wakiwa ni kipa Said Mohammed, beki Salim Mbonde na kiungo Ally Shomary. 
  Mtibwa jana ilishindwa kutwaa Kombe la Mapinduzi 2015 baada ya kufungwa na Simba SC kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
  Kipa Said Mohammed Kasarama alipangua penalti ya Shaaban Kisiga, lakini Ibrahim Rajab ‘Jeba’ akapaisha mkwaju wake na kipa wa Simba SC,
  Ivo Mapunda akaokoa penalti ya mwisho ya Mtibwa iliyopigwa na Vincent Barnabas.
  Penalti za Simba SC zilifungwa na Awadh Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Dan Sserunkuma, wakati za Mtibwa zilifungwa na Aly Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhani Kichuya.
  Hata hivyo, Mtibwa Sugar imetoa kipa bora wa mashindano, Said Mohammed na mchezaji bora Salim Mbonde, huku mfungaji bora ni Simon Msuva wa Yanga SC, mabao manne.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR: KUUZA WACHEZAJI SASA BASI, TUNATAKA MATAJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top