• HABARI MPYA

  Wednesday, January 14, 2015

  MICHO AMTUMIA SALAMU ZA PONGEZI KOCHA MPYA SIMBA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, Miliutin Sredojevic ‘Micho’ amempongeza Mserbia mwenzake, Goran Kopunovic kwa kuanza kazi vizuri Simba SC.
  Kopunovic aliyeanza kazi Januari 2, mwaka huu Simba SC akimpokea Mzambia, Patrick Phiri, jana aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi 2015 kwa kuifunga Mtibwa Sugar kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90.
  “Napenda kutuma salamu za pongezi kwa kocha mpya wa Simba SC, Goran Kopunovic baada ya kuanza kazi vizuri akishinda taji katika wiki ya pili kazini,”amesema Micho.
  Micho amemtumia salamu za pongezi Mserbia mwenzake, Goran Kopunovic kwa kuipa ubingwa Simba SC jana

  “Mafanikio haya ya mapema ni dalili nzuri kwake kwamba atafanya mambo makubwa zaidi Simba SC, kama kocha mwenye taaluma na mchezaji wa zamani, anajua wajibu wake, uimara wa timu yake ni mwanzo wa kupokea changamoto zaidi. Anatakiwa kujiimarisha zaidi,”amesema Micho.
  Kopunovic alishinda mchezo wa tano mfululizo jana tangu aanze kazi Simba SC na baada ya mechi alimkimbilia kipa Ivo Mapunda aliyemuinua benchi dakika ya 90 kwenda kuchukua nafasi ya Peter Manyika, kwa kuokoa penalti ya Vincent Barnabas.
  Awali, Ivo alishuhudia penalti ya Ibrahim Rajab ‘Jeba ikigonga mwamba wakati upande wa Simba SC, penalti ya Shaaban Kisiga ‘Malone’ ilipanguliwa na kipa wa Mtibwa Said Mohammed Kasarama.
  Penalti za Simba SC zilifungwa na Awadh Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Dan Sserunkuma, wakati za Mtibwa zilifungwa na Aly Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhani Kichuya.
  Baada ya mafanikio hayo ya mapema, Mserbia huyo sasa anahamishia mawindo yake katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Jumamosi atasafiri hadi Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kuvaana na wenyeji, Ndanda FC. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MICHO AMTUMIA SALAMU ZA PONGEZI KOCHA MPYA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top