• HABARI MPYA

  Sunday, January 04, 2015

  KOCHA EL MERREIKH ATUA ZANZIBAR KUICHUNGUZA AZAM FC, ATAKUWEPO AMAAN USIKU WA LEO

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  KOCHA wa El Merreikh ya Sudan, Burhan Tia (pichani kulia) amewasili visiwani Zanzibar kwa ajili ya kuwachungunza wapinzani wao katika katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC ya Tanzania Bara.
  BIN ZUBEIRY inafahamu Burhan aliyewasili jana Dar es Salaam, anatarajiwa kuwapo Uwanja wa Amaan, Zanzibar usiku wa leo kuitazama Azam FC ikimenyana na mabingwa wa Zanzibar, KMKM katika mchezo wa Kundi B, Kombe la Mapinduzi.
  Na kocha huyo ataendelea kuwapo Zanzibar ili kuishuhuhudia Azam FC japo katika mechi mbili zaidi, kIsha kurejea Khartoum kuanza kuyafanyia kazi aliyoyaona kwa pamoja na wachezaji wake.
  Wakati Burhan akiwa Zanzibar, kikosi cha Merreikh kimeweka kambi Qatar chini ya kocha wake Mkuu, Mfaransa Diego Garzitto tangu Januari 1 mwaka huu hadi 16, kitakaporejea Sudan kuendelea na maandalizi ya mwisho.
  BIN ZUBEIRY inafahamu, kikiwa Qatar, kikosi cha Merreikh kitacheza mchezo wa kirafiki na Schalke 04 ya Ujerumani Januari 14.  
  Mara ya mwisho zilipokutana katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Merreikh iliitoa Azam FC kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 90 Uwanja wa Nyamirambo, Kigali, Rwanda Agosti mwaka huu.
  Beki wa Merreikh, Ala Eldien Yusif (kushoto) akimdhibiti mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche timu hizo zilipokutana mara ya mwisho Rwanda Agosti mwaka huu

  Baada ya hapo, Azam FC ilisajili mlinzi wa Marreikh, Serge Wawa Pascal raia wa Ivory Coast na ikamkosa kidogo mshambuliaji, Mohamed Traore wa Mali anayechezea timu hiyo pia.
  Azam FC watamenyana na El Merreikh katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Februari 13 na 15 wakati marudiano yatakuwa Februari 27 na Machi 1 na Azam FC wataanzia nyumbani.
  Mshindi baina ya mabingwa hao wa Sudan na Tanzania Bara, atamenyana na mshindi kati ya Lydia Ludic B.A ya Burundi na Kabuscorp do Palanca ya Angola katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA EL MERREIKH ATUA ZANZIBAR KUICHUNGUZA AZAM FC, ATAKUWEPO AMAAN USIKU WA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top