• HABARI MPYA

  Wednesday, January 14, 2015

  KHALID ABEID, TENGA, MOGELLA NA HAO WENGINE WALICHEZA WAPI?

  NASIKIA sikia tu, kwamba miongoni mwa wachezaji wa zamani wa Tanzania wenye maisha mazuri ni Khalid Abeid, Zamoyoni Mogella, Isihaka Hassan ‘Chukwu’ Leodegar Tenga na wengineo.
  Lakini wengi kati ya wanasoka wa zamani, ambao bado gumzo hadi leo maisha yao ni mabovu. Nadhani ni vibaya kusema nani maisha yake mabovu kwa sababu itakuwa sawa na kumdhalilisha.
  Lakini nikitolea mfano wale ambao wameibuka hadharani kutaka msaada kama Christopher Alex Massawe na Jellah Mtagwa haitakuwa dhambi kwa sababu tayari wamekwishajitokeza wenyewe kuomba msaada.

  Lakini ukweli ni kwamba, wale wachezaji nyota alioitwa mashujaa wa taifa wakati fulani, wengi wao wanaishi maisha dhiki na shinda. 
  Kwa ujumla, wanasoka na wanamichezo wengi si hapa Tanzania tu, bali dunia nzima huwa na maisha magumu baada ya kustaafu soka.
  Na kimsingi, maisha rasmi kwa wanamichezo huanza baada ya kustaafu kucheza- ni wakati huo ambao wanaingia kwenye majukumu mazito ya kifamilia.
  Ni wakati huo ambao kwa waliojaaliwa kupata watoto majukumu ya kuwasomesha yanapamba moto.
  Na mbaya zaidi hali hiyo inatokea wakati ambao mchezaji amestaafu mpira na hana chanzo kingine cha maana cha mapato.
  Wachezaji wengi nyota wakati wanacheza, kweli wanapata fedha nyingi kutokana na mishahara, posho na marupurupu mengine, lakini katika maisha yao ya wakati wanacheza wengi huendekeza anasa.
  Kupanga nyumba za gharama kubwa, kununua magari ya kifahari na kutumbua starehe, matokeo yake wanapostaafu soka wanakuwa hawana akiba ya maana na mbaya zaidi hawakukumbuka kuwa na vitegauchumi vyovyote.
  Wengine hulazimisha kuendelea kucheza hata baada ya uwezo kwisha, ili mradi waendelee kupata fedha za kujikimu kimaisha.
  Na wafanye nini, ikiwa familia zinawadai na kwa bahati mbaya wengine hawana ujuzi wala ujanja wa kuishi kwa namna nyingine yoyote.
  Matokeo yake wanaanza kulaani muda waliopoteza wanacheza soka- bora wangefanya shughuli nyingine za kudumu wakawa na msimamo wa muda mrefu wa maisha.
  Hapa Tanzania tunapishana na wanasoka nyota wa miaka iliyopita wakiwa katika hali mbaya za kusikitisha- kwa sababu tu ya kupigika kimaisha.
  Kweli inasikitisha, ukikutana na mtu na ukakumbuka sifa zake wakati wake anacheza na namna alivyo sasa- inatia simanzi.
  Na hiyo si kwenye soka tu, hata wachezaji wa michezo mingine, ikiwemo Netiboli, Ndondi na kadhalika, nao pia wengi wao wanatia huruma na maisha yao.
  Wanasoka wengi ambao wana maisha mazuri ni wale ambao walikwenda shule, ambao baada ya soka walijiendeleza na kuajiriwa.
  Kwa mfano muongo uliopita, wachezaji kama Aaron Nyanda, Ally Mayay, Wilfred Kidau na wengine kadhaa walioshituka mapema na kurejea darasani kuboredsha elimu zao, sasa wana maisha mazuri kwa sababu wana kazi nzuri.
  Wachache waliopata kazi za kutokana na ujuzi kama udereva na Ufundi au kupata bahati ya kuajiriwa viwandani nao angalau wanaendesha maisha.
  Wengine wenye vipaji vya biashara kama Khalid Abeid na Zamoyoni Mogella nao wanaendesha maisha yao vyema, lakini wengine hakika mambo ni magumu na hakuna haja ya kuwataja majina.
  Kilichobaki sasa, wengi wao wanalazimika kubaki kwenye soka, kama makocha au makomandoo kiaina fulani.
  Wakati umefika sasa kizazi kipya cha wanasoka na wanamichezo wa Tanzania wakazingatia kwamba maisha rasmi yanaanza baada ya kustaafu.
  Huo ndiyo wakati ambao majukumu ya kusomesha watoto yanapamba moto na kwa ujumla majukumu ya kifamilia.
  Lazima wachezaji pamoja na kucheza, lakini wakafikiria kuandaa maisha yao ya baadaye.
  Juma Kaseja ni kijana mfano wa kuigwa- mamilioni anayokusanya kwenye soka amekuwa akiwekeza kwenye miradi mbalimbali, ambayo wazi itamsaidia kuendelea kujimudu kimaisha baada ya soka.
  Swali kwa wanasoka wengine ambao wanakusanya mamilioni kwa sasa kama Jonas Mkude na wengine, wanakumbuka kuandaa maisha ya baadaye au ndiyo anasa kwa kwenda mbele?
  Utajenga nyumba, hiyo ni kwa ajili ya kuishi na familia yako, lakini bado kuna maisha ya kila siku ambayo ndani yake kuna kusomesha watoto, umejiandaaje kwa hayo?
  Nani anayeweza kuwapa elimu hii wachezaji wetu ili waepuke maisha magumu baada ya kustaafu soka? Kuna chama cha wachezaji nchini (SPUTANZA) ambacho viongozi wake ni wachezaji wastaafu, wenye uzoefu juu ya hayo, wanawasaidiaje wachezaji wa leo japo kwa kuwaelimisha tu ili wajipange?
  Naamini ipo haja kwa SPUTANZA kuandaa programu maalum kila msimu kutoa elimu kwa wachezaji, japo kwa njia ya vipeperushi ili wajipange kwa maisha ya baadaye.
  Watoe elimu kwa mifano iliyo hai, ili kuwasaidia wanasoka wa kizazi cha sasa na kijacho waweze kujitambua na kujipanga kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. 
  Inawezekana, kwani Khalid Abeid, Mogella, Tenga walicheza wapi? Si hapa hapa Tanzania ambako wachezaji wengine waliocheza nao wamepigika kimaisha! 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KHALID ABEID, TENGA, MOGELLA NA HAO WENGINE WALICHEZA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top