• HABARI MPYA

  Wednesday, January 14, 2015

  IVO: NINGEWAHI KIDOGO KUINGIA, NINGECHEZA PENALTI KIBAO

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  LICHA ya kuokoa penalti moja na kuipa Simba SC ubingwa wa Kombe la Mapinduzi jana, kipa Ivo Mapunda amesema angeweza kuokoa michomo zaidi kama angeingia uwanjani mapema.
  “Nashukuru Mungu nimeokoa penalti na kuipa timu yangu Kombe, kweli mimi ni kipa mzuri na nina uwezo wa kucheza penalti, hilo watu wanalitambua, lakini ni kwa uwezo wa Mungu,”amesema Ivo na kuongeza;
  “Nadhani ningeweza kucheza penalti zaidi kama ningeingia uwanjani mapema, kwa sababu niliingia wakati mchezo unamalizikia. Nilikuwa sijachanganya vizuri. Ndiyo maana nikafanikiwa kucheza penalti ya mwisho kabisa baada ya damu kuchemka kidogo,”amesema.
  Ivo Mapunda wa pili kulia akiwa ameangukiwa na wachezaji wenzake kupongezwa jana
  Ivo akivalishwa Medali na mgeni rasmi jana, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein

  Mapunda alitokea benchi dakika ya 90 kwenda kuchukua nafasi ya Peter Manyika na kuokoa mkwaju wa mwisho uliopigwa na Vincent Barnabas, Simba ikishinda kwa penalti 4-3 baada ya sare ya 0-0.
  Awali, Ivo alishuhudia penalti ya Ibrahim Rajab ‘Jeba ikigonga mwamba wakati upande wa Simba SC, penalti ya Shaaban Kisiga ‘Malone’ ilipanguliwa na kipa wa Mtibwa Said Mohammed Kasarama.
  Penalti za Simba SC zilifungwa na Awadh Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Dan Sserunkuma, wakati za Mtibwa zilifungwa na Aly Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhani Kichuya.
  Ivo alichelewa kujiunga na Simba SC kwa ajili ya mashindano haya kutokana na kuwa na ruhusa maalum ya uongozi wa klabu, kwenda kushughulikia arobaini ya msiba wa mama yake.
  Aliwasili Zanzibar baada ya Simba SC kufika Nusu Fainali na alikuwa benchi siku Wekundu wa Msimbazi wanakata tiketi ya Fainali kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: IVO: NINGEWAHI KIDOGO KUINGIA, NINGECHEZA PENALTI KIBAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top