• HABARI MPYA

  Wednesday, January 07, 2015

  HAJIBU AIPELEKA SIMBA SC NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI KWA HAT TRICK

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MSHAMBULIAJI Ibrahim Hajibu usiku huu ametokea benchi na kuifungia Simba SC mabao matatu katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Taifa ya Jang’ombe Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Simba SC imeshinda 4-0 na hiyo inakua hat trick ya pili katika mashindano haya baada ya awali Simon Msuva wa Yanga kuwafunga hao hao Taifa mabao matatu peke yake katika ushindi wa 4-0 pia, mchezo wa Kundi A.
  Simba SC sasa itasubiri mshindi wa mchezo kati ya mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda na Polisi ya hapa, ikutane naye katika Nusu Fainali Jumamosi.    
  Hajibu aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Juma, alifunga mabao hayo dakika za 46, 63 na 75, kabla ya Shaaban Kisiga ‘Malone’ aliyetokea benchi kufunga la nne dakika ya 80.
  Mshambuliaji wa Simba SC, Elias Maguri akiambaa na mpira usiku huu Uwanja wa Amaan
  Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza Ibrahim Hajibu wa pili kulia

  Hajibu ambaye ni zao la Simba B, alifunga bao la kwanza akimalizia krosi ya Dan Sserunkuma, wakati la pili alimalizia kwa kichwa krosi ya Simon Sserunkuma aliyetokea benchi pia.
  Bao la tatu Hajibu alifunga kwa penalti baada ya yeye mwenyewe kuangushwa kwenye eneo la hatari na Abdallah Hajji. Malone alifunga bao lake kwa shuti la mpira adhabu baada ya yeye mwenyewe kuangushwa umbali wa mita 26.  
  Baada ya mchezo, beki wa kulia wa Simba SC, Hassan Kessy alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi na kuzawadiwa na Azam TV.
  Robo Fainali nyingine zinatarajiwa kuchezwa kesho, kati ya KCCA na Polisi, Azam FC na Mtibwa Sugar na Yanga na JKU. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy/Said Nassor ‘Chollo’ dk81, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’/Shaaban Kisiga ‘Malone’ dk66, Said Ndemla/Abdallah Seseme dk81, Elias Maguri, Dan Sserunkuma na Awadh Juma/Ibrahim Hajibu dk46.
  Taifa; Kassim Abdallah, Omar Yussuf, Hafidh Bakari, Khamis Ali, Abdallah Hajji, Hassan Said, Hassan Barik, Hassan Nassor, Abdul Seif, Abdallah Mudhihir na Shaib Seif. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAJIBU AIPELEKA SIMBA SC NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI KWA HAT TRICK Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top