• HABARI MPYA

  Monday, January 05, 2015

  COUTINHO: SASA SHWARI KABISA YANGA SC

  Na Mahmoud Zubeiry, ZANZIBAR
  MBRAZIL Andrey Coutinho amesema kwamba mabao mawili aliyofunga jana Yanga SC ikishinda 4-0 dhidi ya Polisi katika mchezo wa Kundi A, Kombe la Mapinduzi yamemrejeshea hali ya kujiamini.
  Coutinho alifunga bao la kwanza na la tatu jana Uwanja wa Amaan, Zanzibar  Yanga SC ikijikatia tiketi ya kutinga Robo Fainali Kombe la Mapinduzi, mabao mengine yakifungwa na Mliberia Kpah Sherman na Simon Msuva.
  “Nimefurahi sana kufunga mabao mawili leo, imenirejeshea hali ya kujiamini. Najua kuna wakati sichezi vizuri, lakini wakati mwingine nacheza vizuri, tena sana,”.
  Andrey Coutinho baada ya kuifungia Yanga SC mabao mawili jana Uwanja wa Amaan

  “Hiyo ni hali ya kawaida kwa kila mchezaji, hakuna mchezaji anayeweza kucheza vizuri siku zote. Mashabiki lazima waelewe hicho kitu. Watu walikwishaanza kunichukulia kama mimi si mchezaji mzuri, lakini nimewadhihirishia,” amesema.
  Coutinho amewataka mashabiki wa Yanga SC wajifunze kuwavumilia wachezaji wakati ambao hawachezi vizuri, kwani ni hali ambayo inaweza kumtokea mchezaji yeyote duniani.
  Coutinho jana alifunga kwa mara ya kwanza tangu Septemba 28, mwaka jana alipoifungia Yanga bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kwa ujumla Coutinho sasa ana mabao manne katika mechi 13 alizocheza Yanga SC hadi sasa, matatu akifunga Uwanja wa Amaan. 
  Coutinho alisajiliwa kwa pamoja na Mbrazil, mwenzake Genilson Santana Santos ‘Jaja’ Julai mwaka jana Yanga SC, lakini mwenzake huyo aliondoka mwishoni mwa mwaka baada ya kucheza mechi 11 na kufunga mabao matano.
  Wawili hao wote waliletwa na kocha Mbrazil mwenzao, Marcio Maximo ambaye naye amefukuzwa Desemba pamoja na Msaidizi wake, Leonardo Leiva.
  Maximo alileta kiungo mwingine Mbrazil, Emerson de Oliviera Roque Desemba azibe nafasi ya Jaja, lakini Yanga SC iliachana naye baada ya mechi moja ya Mtani Jembe, wakifungwa 2-0 na watani Simba SC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: COUTINHO: SASA SHWARI KABISA YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top