• HABARI MPYA

  Friday, January 09, 2015

  CDS YALETA BONANZA LA MIAKA 10 LEADERS

  KAMPUNI ya CDS  imeandaa mashindano maalumu  ya kusherehekea  miaka 10, huku timu nane za makampuni na taasisi mbalimbali zikishirikishi mashindano hayo yanayoanza kutimua vumbi kesho viwanja vya Leaders Dar es Salaam .
  Akizungumza na waandishi wa Habari, Dares Salaam jana,  Meneja Mkuu wa CDS, Juma Uledi, alisema kuwa timu hizo zitashindana katika mchezo wa soka na watachuana kwa njia ya mtoano ambapo fainali zake zitafanyika Januari 23 mwaka huu.
  Meneja Mkuu wa CDS, Juma Uledi, wa nne (kushoto)akiwa na viongozi wa timu zinazoshiriki bonanza maalumu la miaka 10 ya kampuni hiyo, linaloanza kutimua vumbi kesho kutwa, kwenye viwanja wa Leaders Club  

  Uledi alizitaja timu zitakazoshiriki mashindano hayo ni pamoja na Vodacom, benki ya BOA, Tanzania Stars, Zantel, Clouds Media, Bongo Movie, Global Publishers na wenyeji CDS.
  Uledi alisema kuwa mbali na michuano hiyo ya soka, pia wameandaa bonanza la burudani ' Usiku wa CDS' ambalo litafanyika  siku ya kilele cha sherehe hizo 
  kwenye viwanja vya TCC, Sigara Chang'ombe.
  "Pia tumepanga kutoa nafasi kwa wadau wetu kutangaza huduma wanazotoa kwa umma siku hiyo ya kilele kuanzia saa moja asubuhi hadi saa moja usiku," alisema meneja huyo wa kampuni hiyo inayojihusisha na kusafirisha mizigo.
  Alizitaja bendi zitakazotoa burudani siku hiyo kuwa ni Malaika, FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma', Papacha Watatu, Msondo Ngoma na mkongwe wa muziki wa taarab, malkia, Khadija Kopa.
  Alisema pia wanatarajia kufanya mashindano hayo kila mwaka na wataongeza michezo ili kutoa nafasi kwa wadau wao mbalimbali kushiriki sherehe hizo. Timu zote nane jana zilikabidhiwa jezi kwa ajili ya kuzitumia kwenye michuano hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CDS YALETA BONANZA LA MIAKA 10 LEADERS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top