• HABARI MPYA

  Monday, January 19, 2015

  BOCCO AREJEA DAR, ‘DILI LIMEBUMA’ ALGERIA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ amerejea Dar es Salaam kutoka mjini Ain Fakroun, Algeria alipokwenda kwa mipango ya kujiunga na klabu ya Chabab Riadhi Baladiyat, maarufu kama CRB. 
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zinasema kwamba, Bocco amerejea baada ya kushindwa kufikia makubaliano na klabu hiyo inayovalia jezi za rangi nyeusi na nyeupe. 
  Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba amekiri kurejea kwa Bocco na amesema ataungana na timu mjini Mwanza mapema kwa ajili ya mchezo na Kagera Sugar kesho.
  Bado haijajulikana sababu ya kutofikiwa maafikiano ni Bocco au uongozi wa timu hiyo ya Daraja la Kwanza Algeria, maarufu kama Professionnelle 2.
  John Raphael Bocco 'Adebayor' amerejea nyumbani baada ya mipango ya kuhamia Algeria kukwama

  Msimu wa 2012–13, CRB Ain Fakroun ilishika nafasi ya kwanza katika Professionnelle 2 na kufanikiwa kupanda Ligi Kuu ya Algeria ijulikanayo kama Professionnelle 1 kwa mara ya kwanza, kabla ya kushuka tena.
  Iwapo mpango wa Bocco aliyezaliwa Agosti 5, mwaka 1989 kuhamia Algeria utakwama moja kwa moja, hii itakuwa mara ya tatu kujaribu bila mafanikio kwenda kucheza nje, baada ya awali kufanya majaribio Afrika Kusini na Israel, ambako licha ya kuelezwa alifuzu, lakini biashara haikufanyika.
  Awali, Bocco alifanya majaribio kwa wiki kadhaa katika klabu ya Ligi Kuu Israel mwaka 2010 na baadaye Afrika Kusini katika klabu ya Supersport United.
  Bocco alifuzu Supersport baada ya wiki mbili, lakini Azam FC ikagoma kumuuza kwa sababu ya dao dogo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOCCO AREJEA DAR, ‘DILI LIMEBUMA’ ALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top