• HABARI MPYA

  Saturday, January 03, 2015

  ‘BEKI LA SIMBA’ LAELEKEA ZESCO UNITED YA ZAMBIA

  Na Vincent Malouda, NAIROBI
  BAADA ya Simba SC kukosa kumsajili beki wa Gor Mahia David ‘Calabar’ Owino katika dirisha fupi la uhamisho nchini Tanzania, klabu ya ligi kuu ya Zambia Zesco United sasa imo mbioni kumnasa mchezaji huyo wa timu ya taifa la Kenya, Harambee Stars.
  Katibu mkuu wa Zesco United Justin Mumba ameliambia BIN ZUBEIRY kwa njia ya simu kutoka makao makuu ya klabu hiyo, Ndola, kwamba wanamtarajia beki huyo jumatatu tarehe 5 kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kumwaga wino kwenye karatasi.
  “Tayari tushazungumza na wakala na klabu yake na kinachosalia ni yeye kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kusaini mkataba wowote japo tushamjumuisha kwenye kikosi chetu cha muda cha kombe la klabu bingwa barani Afrika mwaka huu, alisema Mumba.
  David Owino 'Calabar' alikaribia kutua Simba SC Desemba mwaka jana

  BIN ZUBEIRY imeelezwa na kiongozi mmoja wa Gor Mahia kuwa Zesco United inarajia kutoa kitita cha dola za marekani 35 000 ambapo Gor Mahia itapokea dola 15 000 huku Owino, 26, akitia mfukoni dola 20 000.
  Owino ambaye ameshinda tuzo za beki bora nchini Kenya misimu miwili iliyopita amecheza mechi 33 mwaka huu; 26 za ligi kuu, tatu kwenye taji la nane bora na nne kwenye kombe la CECAFA Kagame Cup na kufunga mabao mawili ya ligi dhidi ya KCB na Ulinzi Stars.
  Ameichezea timu ya taifa Harambee Stars mara 30 na kufunga mabao mawili kufikia sasa, moja dhidi ya Namibia kwenye michuano ya kufuzu kombe la dunia 2014.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ‘BEKI LA SIMBA’ LAELEKEA ZESCO UNITED YA ZAMBIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top