• HABARI MPYA

  Tuesday, January 20, 2015

  AZAM FC YARUDI KILELENI LIGI KUU, YAICHAPA 3-1 KAGERA SUGAR KIRUMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, MWANZA
  AZAM FC imerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jioni ya leo.
  Kwa matokeo hayo, mabingwa hao watetezi wanatimiza pointi 20 baada ya kucheza mechi 10, tatu zaidi ya Mtibwa Sugar wanaoshika nafasi ya pili, lakini wana mechi moja mkononi.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Jacob Adongo wa Mara aliyesaidiwa na Charles Simon wa Dodoma na Robert Luhemeja wa Mwanza,  hadi mapumziko tayari Azam FC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
  Wachezaji wa Azam FC wakicheza kushangilia bao lao la kwanza lililofungwa na Kipe Tchetche wa pili kushoto
  Kipre Tchetche (kulia) akimlamba chenga Abubakar Mtiro kabla ya kufunga bao la kwanza

  Mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche alifunga bao la kwanza dakika ya tatu, baada ya kumlamba chenga beki mkongwe Abubakar Twaha Mtiro, kufuatia pasi ya Frank Domayo na kumchambua kipa Agathon Anthony kwa guu la kushoto.
  Bao la pili lilifungwa na mshambuliaji Mrundi, Didier Kavumbangu kwa shuti la guu la kulia, aliyemalizia krosi ya Kipre Tcheche, ambaye alipasiwa na Erasto Edward Nyoni pembeni kushoto.
  Kagera Sugar walizidiwa kipindi cha kwanza, lakini kwa mashambulizi yao machache ya kushitukiza walikaribia kufunga mara mbili, kwanza dakika ya 12 shuti la Atupele Green lilipodakwa na kipa Aishi Manula na baadaye dakika ya 38, ilipotokea piga nikupigie langoni mwa Azam, kabla ya Shomary Kapombe kuokolea mpira kwenye mstari.
  Kipindi cha pili, Kagera Sugar walikanza vizuri wakifanikiwa kupata bao dakika ya 55, mfungaji  Rashid Mandawa.
  Hata hivyo, Azam walizinduka na kuongeza mashambulizi hadi kupata la tatu dakika ya 67, mfungaji Kavumbangu tena aliyemalizia krosi ya Mganda Brian Majwega.
  Baada ya bao hilo, Azam FC ilitengeneza nafasi zaidi, lakini ikashindwa kuzitumia, huku Kagera wakizidi kupoteana uwanjani.
  Kikosi cha Kagera Sugar kilikuwa; Agatony Anthony, Benjamin Asukile, Abuu Mtiro, Eric Kyaruzi, Ibrahim Job/Shai Mpala dk57, George Kavilla, Juma Mpola, Babu Ally/Paul Ngway dk30, Rashid Mandawa, Daudi Jumanne ‘Dunga’ na Atupele Green/Adam Kingwande dk79. 
  Azam FC; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Said Mourad, Serge Wawa, Kipre Balou, Mudathir Yahya, Frank Domayo/Himid Mao dk53, Didier Kavumbangu/Gaudence Mwaikimba dk76, Kipre Tchetche/Amri Kiemba dk85 na Brian Majwega. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YARUDI KILELENI LIGI KUU, YAICHAPA 3-1 KAGERA SUGAR KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top