• HABARI MPYA

    Saturday, November 10, 2012

    KIGOGO WA SIMBA AWAPONZA WACHEZAJI WANNE 'KUPOTEZA MAISHA' AZAM

    Aggrey Morris

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIPA Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris sasa watabaki historia katika klabu ya Azam FC, kufuatia msimamo wa Menejimenti ya timu hiyo, kuwafukuza moja kwa moja baada ya kuwakuta na tuhuma za kuhujumu timu hiyo.
    Wachezaji hao, wakiongozwa na Nahodha wao, Morris inadaiwa walipokea rushwa kutoka kwa kiongozi wa juu kabisa wa klabu ya Simba, ambaye ukitajiwa huwezi kuamini ili kuihujumu timu hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Aggrey aliondolewa kambini jana, siku moja tu baada ya kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Said Mourad na Erasto Nyoni nao kusimamishwa kwa tuhuma hizo.
    Azam ilifungwa na Simba mabao 3-1 Oktoba 27, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi za Ligi Kuu na baada ya hapo ikamfukuza kocha wake Mserbia, Boris Bunjak na kumrejesha Muingereza, Stewart Hall.
    Habari kutoka ndani ya Azam zimesema kwamba baada ya kupata taarifa hizo, uongozi ulizifanyia kazi kwa kushirikisha hadi na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ambayo imekamilisha uchunguzi na ripoti imewataja wachezaji hao wanne kupokea rushwa kutoka kwa bosi huyo wa Simba.
    Hata hivyo, Dida hakucheza mechi hiyo, kwani Oktoba 27, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad, Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz aliyempisha Abdi Kassim, Himid Mao aliyempisha Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’ aliyempisha Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Herman Tcheche na Salum Abubakar.
    Siku hiyo, Azam walitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja, kabla ya Felix Mumba Sunzu Jr., kuisawazishia Simba dakika mbili baadaye, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
    Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto na dakika tano tu tangu kuanza kipindi cha pili, Mganda huyo tena akawainua vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa Azam.
    Azam ambayo leo inamenyana na Mgambo JKT, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kutokana na uhaba wa mabeki wa kati, italazimika kutumia mabeki wa pembeni katikati leo ambao ni Luckson Kakolaki na Samir Hajji Nuhu kuziba mapengo ya Mourad na Morris. Aidha, katika beki ya kulia atacheza kiungo mshambuliaji, Kipre Balou.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KIGOGO WA SIMBA AWAPONZA WACHEZAJI WANNE 'KUPOTEZA MAISHA' AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top