• HABARI MPYA

    Saturday, November 10, 2012

    SIMBA INA KAZI NA TOTO LA YANGA LEO, AZAM NA MIGAMBO TANGA

    Wachezaji wa Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unakamilishwa wikiendi hii, leo na kesho kwa mechi saba kuchezwa katika viwanja tofauti.
    Mabingwa watetezi, Simba watakuwa wenyeji wa Toto Africans ya Mwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo JKT wataikaribisha Azam FC Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Lyon na Mtibwa Sugar Chamazi, Dar es Salaam, Prisons na JKT Ruvu Sokoine, Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro, Kaitaba, Bukoba na JKT Oljoro na Ruvu Shooting Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha leo.
    Simba wanahitaji ushindi leo kurejesha matumaini ya ubingwa- na pia kutuliza hali fulani ndani ya klabu yao, baada ya kufungwa na Mtibwa Sugar 2-0 katika mchezo wake uliopita.
    Nahodha wa Simba, Juma Kaseja alifanyiwa fujo na mashabiki baada ya mechi hiyo na kuamua kususia mazoezi wiki yote hii, wakati wanachama waliandamana na mabango hadi makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi wakisema wanataka Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Kaseja wajiuzulu.
    Simba imekuwa ikijifua Uwanja wa Kinesi kwa wiki yote hii na imeweka kambi katika hoteli ya Suphire, Karakoo. Mbali na Juma Kaseja, beki Amir Maftah hayuko kambini pia, kwa sababu ni majeruhi na bado anakula fungate la ndoa yake, wakati huo huo beki Juma Nyosso na kiungo Haruna Moshi wanaendelea kutumikia adhabu ya kusimamishwa.
    Bila shaka kesho, Wilbet Mweta atadaka dhidi ya timu yake ya zamani leo wakati kikosini wengine watakuwa Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Felix Sunzu na Emanuel Okwi.   
    Toto; Erick Ngwengwe, Kulwa Greyson, Eric Mulilo, Evarist Maganga/Heri Kyaruzi, Peter Mabula, Hamisi Msafiri, Emanuel Swita, Haroun Athumani, Mohamed Hussein, Suleiman Kibuta na Mussa Said/Heri Mohamed. 
    Toto African imejichimbia eneo la Tandika mjini Dar es Salaam kwa takriban wiki nzima, ikijifua vikali tayari kwa mchezo wao dhidi ya Simba leo.
    Lakini kocha wake, John Tegete yeye hakuja Dar es Salaam kwa sababu ya majukumu ya kitaifa, anashughulikia maandalizi ya mechi ya kirafiki ya Taifa Stars na Harambee Stars.
    Azam wanaingia kwenye mechi  ya leo baada ya kuwasimamisha wachezaji wake wanne, kipa Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Erasto Nyoni, Aggrey Morris na Said Mourad, kwa tuhuma za kuhujumu timu hiyo kwenye mechi dhidi ya Simba Oktoba 27, mwaka huu.
    Azam inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu kwa pointi zake 24, wakiizidi Simba pointi moja na wakishinda leo watapanda kileleni hata kama Simba itaifunga Toto.
    Azam wanaweza kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa kileleni, iwapo Yanga haitashinda dhidi ya Coastal kesho. 
    Yanga iliondoka jana alfajiri Dar es Salaam kwenda Tanga, tayari kwa mechi na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumapili.
    Msafara wa timu hiyo ukiwa njiani eneo la Kabuku, gari lao lilitupiwa jiwe na mtu anayedhaniwa kuwa ni shabiki wa Simba na kupasuka kioo. Hata hivyo, hakuna mtu aliyeumia.
    Yanga imepania kushinda mechi hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri katika msimamo wa Ligi Kuu, ambayo mzunguko wake wa pili utarejea Januari mwakani.
    Yanga ilifanya mazoezi yake ya mwisho juzi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam na wachezaji wake wote wapo vizuri, chini ya kocha wake Mholanzi, Ernie Brandts.
    Wchezaji wa Yanga wamepania kuvunja rekodi ya Coastal Union kutofungwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani, Mkwakwani, Tanga katika mechi hiyo.
    Nahodha Msaidizi wa Yanga, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ alisema kwamba wanataka kustawisha uongozi wao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kuwafunga Coastal Jumamosi.
    Alisema wanajua Coastal ni timu nzuri na wanatarajiwa upinzani katika mechi hiyo, ila ameonya Yanga ya sasa ni tishio na wachezaji wako vizuri ‘ile mbaya’.
    Lakini pia habari za ndani kutoka Yanga zinasema kwamba tayari wachezaji wameahidiwa donge nono iwapo watashinda mechi hiyo.
    Wachezaji hao, walizawadiwa Sh. Milioni 15 kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 26 na ikishinda dhidi ya Coastal itakwenda kupumzika kwa raha sana. 
    Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal, Nassor Bin Slum amesema Yanga watake wasitake watafungwa Mkwakwani Jumapili. Msimu uliopita, Yanga waliifunga Coastal mechi zote, kwanza 5-0 Dar es Salaam na 1-0 Tanga.
    Lakini Coastal ya mwaka huu ni nyingine kabisa, kwani imesajili wachezaji wazuri na wazoefu. Nsa Job hatakuwapo kwa sababu anaumwa goti, lakini yupo mkali mwingine wa mabao katika timu hiyo, Daniel Lyanga.
    Burudani zaidi inatarajiwa kuwa katika safu ya kiungo, Coastal kuna Razack Khalfan na Jerry Santos na Yanga wapo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima. Yanga wameshinda mechi mbili za ugenini kati ya tano, wametoa sare moja, wamefungwa mbili pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA INA KAZI NA TOTO LA YANGA LEO, AZAM NA MIGAMBO TANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top