![]() |
| Samatta ataiongoza Mazembe dhidi ya wenye Kombe leo Lubumbashi |
Na Prince Akbar
MABINGWA
mara sita Afrika, Al Ahly ya Misri wamelazimishwa sare ya kufungana mabao 3-3 na
Sunshine Stars ya Nigeria katika mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa
Afrika jana iliyopigwa huko Ijebu-Ode kwenye Uwanja wa kimataifa wa Dipo Dina.
Nahodha wa Sunshine,
Godfrey Oboabona aliikosa mechi hiyo baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano katika
mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya Esperance ya Tunisia, wakati Mohamed Aboutrika
anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi miwili na Ahly.
Ahly ilipata
bao la kwanza dakika ya 18 kupitia kwa Mohamed Nagy, aliyefumua shuti kutoka
nje ya boksi na kumtungua Moses Ocheje, kabla ya Mahdy El Sayed kuifungia bao
la pili timu hiyo dakika ya 30, wakati Sunshine ilipata bao la kwanza dakika ya
40, kupitia kwa kiungo Mcameroon, Tamen Medrano aliyemtungua kwa shuti la mbali
kipa wa Ahly, Sherif Elkramy.
Wenyeji walisawazisha
dakika ya 73 kwa mkwaju wa penalti wa Dele Olorundare baada ya Ajani Ibrahim kuangushwa
kwenye eneo la hatari na Mohamed Nagy.
Pamoja na
hayo, Mashetani Wekundu wa Cairo walipata bao lililoelekea kuwa la ushindi, dakika
moja badaaye kupitia kwa kijana mwenye umri wa miaka 25, Nagy ambalo lilikuwa bao
lake la pili kwenye mechi hiyo.
Beki wa Sunshine,
Precious Osasco aliisawazishia timu yake dakika ya 83 kwa shuti la mpira wa
adhabu lililomshinda kipa Elkramy. Nagy alipata
nafasi ya kukamilisha hat-trick dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho, lakini
kichwa chake kiliupaisha mpira alipokuwa anaunganisha kona.
Mechi ya
marudiano itachezwa wiki ijayo Cairo katika Uwanja ambao mashabiki hawataingia
na mshindi wa jumla atamenyana na mshindi kati ya mabingwa watetezi, Esperance na
TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ikiongozwa na
washambuliaji wawili chipukizi wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas
Ulimwengu, leo Mazembe itaikaribisha Esperance mjini Lubumbashi katika Nusu ya
Fainali ya pili.



.png)
0 comments:
Post a Comment