• HABARI MPYA

    Sunday, October 07, 2012

    SIMBA WALEEEEE, KIEMBA APIGA MBILI OLJORO IKITANDIKWA 4-1

    Edward Christopher kushoto akimpongeza Kiemba aliyepiga mbili leo
    Na Mahmoud Zubeiry
    SIMBA SC imezidi kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 4-1 ilioupata jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
    Katika mechi hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya 29.
    Kiemba alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na mashambulizi ya upande wa kulia.
    Ilikuwa rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
    Nonga naye alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni kiulaini.
    Bao hilo lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
    Kipindi cha pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao mawili zaidi.
    Dakika ya 83 Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango huyo.
    Awali ya hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao la nne kwa mkwaju wa penalti.
    Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi tano.
    Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Paul Ngalema/Kiggi Makassy, Shomary Kapombe, Juma Nyosso, Amri Kiemba, Jonas Mkude/Daniel Akuffo, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Edward Christopher/Haruna Moshi na Emmanuel Okwi.
    JKT Oljoro; Shaibu Issa, Yussuf Nachogote, Nafo Zuberi/Jackson Semfukwe, Salim Mbonde, Marcus Raphael (Nahodha), Emanuel Memba, Karage Gunda, Saleh Iddi/Amir Omar, Paul Nonga, Meshack Nyambele na Sixbert Mohamed/Essau Sanu. 
    Wachezaji wa Simba 

    JKT Oljoro wakiomba dua

    Kipa wa Oljoro, Shaibu Issa akidaka mbele ya Edward Christopher

    Edward Christopher kulia akimnyatia kipa wa Oljoro, Shaibu Issa

    Edward Christopher akichanja mbuga

    Emanuel Okwi akipasua msitu wa mabeki

    Edward Chiristopher akisafiri

    Simba wakishangilia
    Kiemba anafunga


    Kiemba anashangilia
    Mkude anampogeza Kiemba


    Kikosi cha JKT Oljoro leo

    Juma Nyosso

    Kocha wea Oljoro, Mbwana Makatta

    Jonas Mkude

    Kikosi cha Simba leo

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA WALEEEEE, KIEMBA APIGA MBILI OLJORO IKITANDIKWA 4-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top