![]() |
| Simba SC |
Na Prince Akbar
LIGI Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, inataraiwa kuendelea leo kwa mabingwa watetezi na vinara
wa ligi hiyo, Simba kuumana na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mchezo ambao
unatarajiwa kuwa mkali na wa kusimua.
Katika mchezo
huo, Simba SC itawakosa wachezaji wake wanne, wakiwemo beki Shomary Kapombe
aliyeumizwa na mshambuliaji Said Bahanuzi wa Yanga Jumatano na Mrisho Ngassa,
ambaye ana Malaria.
Ofisa Habari
wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga alisema jana katika Mkutano na Waandishi wa
Habari, makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi kwamba, mbali na nyota hao
wawili, wengine watakaokosekana kwenye mechi ya leo ni mabeki Amir Maftahi
anayetumikia adhabu ya kadi na Haruna Shamte, ambaye pia ni majeruhi.
Kamwaga
alisema kwamba Kapombe aliumizwa na mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi
Jumatano katika mechi baina ya watani hao wa jadi wa soka ya Tanzania,
iliyopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya 1-1.
Kuhusu
Ngassa, Kamwaga alisema kwamba baada ya mechi hiyo ya Jumatano, naye amepata
Malaria, ambayo itamuweka nje ya Uwanja kesho, wakati Haruna aliumia mazoezini,
timu hiyo ilipokuwa kambini Zanzibar ikijiandaa na mechi ya Yanga.
Lakini
Kamwaga alisema pamoja na kuwakosa nyota hao, anaamini wachezaji wengine
watakaochukua nafasi zao watafanya vizuri. Kumbuka Emmanuel Okwi amemaliza
adhabu na kesho anaweza kuiongoza Simba kwenye mechi hiyo.
Mechi ningine
za leo ni kati ya vibonde wa ligi hiyo, Mgambo Shooting watakuwa wenyeji wa
vibonde wengine wa ligi hiyo, Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini
Tanga, wakati Toto Africans wataikaribisha JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Kirumba mjini
Mwanza na Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa
Sokoine mjini Mbeya.
Kagera Sugar
wataikaribisha Yanga kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kesho. Hadi sasa,
mwenendo wa ligi unaonyesha ushindani ni kati ya mabingwa watetezi, Simba SC na
washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC ambazo zinakabana kileleni.
Hali bado si
nzuri kwa mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga SC ambayo inazidiwa pointi
tano na mabingwa watetezi, Simba SC ambao pia ni wapinzani wao wa jadi.
Timu mbili
kati ya tatu zilizopanda Ligi Kuu msimu huu JKT Mgambo na Polisi Morogoro ndizo
zipo mkiani, wakati Prisons ndio inaonekana kuwa imara zaidi, kwani ipo nafasi
ya tano katika msimamo huo.
Katika mechi
za jana, Azam FC iliisogelea zaidi Simba kileleni mwa Ligi Kuu baada ya
kuifunga African Lyon bao 1-0 kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Azam ambayo
ilimaliza mechi hiyo ikiwa pungufu ya mchezaji mmoja, baada ya beki wake, Samir
Hajji Nuhu kutolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 83 kwa kuonyeshwa kadi ya
pili ya njano, imefikisha pointi 13 sawa mabingwa watetezi Simba, ambao wapo
kileleni sasa kwa wastani wa mabao tu.
Hadi
mapumziko, Azam walikuwa tayari mbele kwa bao hilo, lililotiwa kimiani na
mfungaji bora wa Ligi Kuu, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ katika dakika ya
kwanza ya muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Hilo
linakuwa bao lake la pili Adebayor msimu huu ndani ya mechi tano za Ligi Kuu,
hali ambayo inaashiria kasi yake yake si ya kuridhisha msimu huu.
Kikosi cha
Azam kilikuwa; Mwadini Ally, Erasto Nyoni, Samir Hajji Nuhu, Aggrey Morris,
Said Mourad, Ibrahim Mwaipopo/Salum Abubakar dk57, Jabir Aziz, Himid
Mao/Abdulhalim Humud dk60, John Bocco ‘Adebayor’m, Kipre Tcheche na Abdi Kassim
‘Babbi’.
Katika
mchezo mwingine jana, wenyeji Ruvu Shooting wameifunga Coastal Union ya Tanga mabao
2-0 kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani, mabao yaliyotiwa
kimiani na Hussein Sued dakika ya sita na Hassan Dilunga dakika ya 12.



.png)
0 comments:
Post a Comment