• HABARI MPYA

    Wednesday, June 20, 2012

    CHEZEENI YOTE, VYOTE LAKINI SI JINA LA TIMU YA TAIFA


    Na Mahmoud Zubeiry

    GUMZO kubwa kwa sasa katika soka ya Tanzania, ukiacha kutolewa kwa timu zetu zote za taifa, wanawake za wanaume katika kinyang’anyiro cha tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika, ni kuhusu jina la timu ya wanaume, Taifa Stars.
    Baada ya kupata wadhamini wapya, Kilimanjaro Beer, kumekuwa kuna mpango wa kuibadilisha timu hiyo, ibebe jina la wadhamini, Kilimanjaro Beer. Tayari baadhi ya vyombo vya habari vimekwishaanza kuitambulisha timu hiyo kama Kilimanjaro Taifa Stars.
    Nani anajua jina la Taifa Stars lilianzia wapi? Nilimuuliza Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah Tenga wiki iliyopita, alisema hajui bali anachokumbuka tangu anaanza soka amekuwa akilisikia jina hilo.
    Jina hili ni mseto mzuri wa lugha mbili ambazo ni asili haswa ya Tanzania, kwanza Kiswahili chetu (Taifa) na pili Kiingereza (Stars) kwani taifa letu lilipokea Uhuru wake kutoka kwa Muingereza.
    Kuanzia shule ya Msingi, Watanzania wanasoma Kiswahili na Kiingereza na hizo ndizo lugha zetu, maana yake, nyota wa taifa. Ndiyo, timu ya taifa ni mseto wa wachezaji nyota katika taifa letu kutoka timu tofauti.
    Watanzania, wengi wetu tunapenda kubabaikia vitu vya wenzetu na hatupendi kabisa kuthamini vilivyo vya kwetu- jambo ambalo ni hatari sana kwa maendeleo ya taifa letu. Kwa sababu ya kupenda vya wenzetu, wapo wanaotamani majina ya timu yetu yatokane na majina ya timu nyingine, zikiwemo za Ulaya. Inasikitisha.
    Tanzania itabakia kuwa Tanzania tu kwa asili yake inayotokana na muungano wa mataifa mawili, Tanganyika na Zanzibar- hivyo kuthubutu kubabaikia vitu vya wengine huo ni utumwa wa kifikra.
    Tazama kila kitu leo Tanzania ni mfano wa vitu vya nje hususan Magharibi, na mbaya zaidi hii inaanzia hadi kwenye vyombo vya habari. Mfumo wa kurasa, vipindi vya radio na Televisheni zetu ni Umagharibi mtupu.
    Tunakosa fursa ya kuipromoti nchi yetu na vilivyo vyetu kutokana na utumwa huu. Hatuna vipindi vya kusaidia kuitangaza nchi yetu na bado tunatarajia kuvutia watalii kwa wingi nchini mwetu.
    Taifa Stars enzi za Ally Hassan Mzee Mwinyi rais wa Tanzania, leo inataka kubadilishwa jina.
    Kutwa nzima Radio na TV wanapiga nyimbo za wasanii wa nje, filamu za nje na kwa sababu hiyo hata wasanii nao, wanalazimika kufanya vitu kwa kuiga nje, ili wapate sehemu ya kupromoti kazi zao.
    Lakini hatujiulizi kwa nini Wakongo wanaimba Kilingala au Wanigeria wanaigiza katika mazingira yao na asili yao kwa kiasi kikubwa.
    Kwa sababu hiyo hiyo, tunaona sasa Taifa Stars halifai na tunataka jina mbadala- badala ya kufikiria namna gani tutafanya ili soka letu likue, nasi tuwe tunashiriki michuano mikubwa, tunapoteza muda kujadili jina. Jina halichezi mpira.
    Lakini pamoja na shinikizo la kubadili jina kwa sababu ya ubabaikaji wetu, pia kuna shinikizo la wadhamini wapya. Jina la timu ya taifa si la kuchezea. Wadhamini wapya wafanye wanavyoweza kufanya kuitumia timu ya taifa kujinufaisha kibiashara, lakini si kwa kubadili jina.
    Watu wengi wa Idara za Masoko nchini bado mitazamo yao ni finyu na wanafanya kazi kwa mazoea na kukariri- wanaamini kukipa jina la bidhaa yako kitu unachodhamini ndio inaleta maana na faida kumbe sivyo.
    Taifa Stars katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu wa
    zamani Tanzania, 'Simba wa Vita' marehemu Rashid Mfaume Kawawa,
    leo inataka kubadilishwa jina, je ni sahihi kweli?
    Unaweza kufanya promosheni nzuri kupitia kitu unachokidhamini na ukanufaika kwa kiasi kikubwa. Na pia unaweza kuibadilisha timu ya taifa na kuipa jina lako la bidhaa yako, lakini bado usinufaike ikiwa hauna mipango mizuri ya promosheni.
    Wenzetu Kenya timu yao ya taifa inadhaminiwa na Tusker Beer, lakini bado inaitwa Harambee Stars. Ila Tusker inaendelea kunufaika na udhamini wao kutokana na mipango madhubuti ya promosheni waliyojiwekea.
    Cameroon wamebadilisha wadhamnini wangapi tangu mwaka 1992 wacheze Robo Fainali ya Kombe la Dunia na bado timu yao inaitwa Indominatable Lions tu? Nigeria kadhalika, ilibadilika jina mara moja tu kutoka Green Eagles hadi Super Eagles ila pamoja na kubadilisha wadhamini kibao wa timu ya taifa, bado jina ni lile lile tangu marehemu Rashid Yekini anacheza hadi leo John Obi Mikel.
    Mambo matatu nataka kusema, kwanza kwa mashabiki wenye fikra za kitumwa kwa kubabaikia majina ya nje, waondokane na fikra hizo- pili kwa wadhamini Kilimanjaro Beer, waketi chini na kutafakari namna ya kunufaika na udhamini wao kwenye timu hiyo bila kuchezea jina ambalo muasisi wa taifa hili, marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliacha na tatu ni kwa TFF, wasithubutu kuchezea jina la timu ya taifa. Historia itawahukumu. Nawasilisha!
    Kikosi cha sasa Taifa Stars, je Watanzania watakubali jina la timu libadilike?

         
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHEZEENI YOTE, VYOTE LAKINI SI JINA LA TIMU YA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top