• HABARI MPYA

    Friday, September 02, 2016

    STARS TAYARI KUUA TAI MKUBWA WA NIGERIA KESHO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kesho Septemba 3, 2016 inatarajiwa kuingia kibaruani kwa kucheza na Super Eagles ya Nigeria katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017).
    Mchezo huo utafanyika kuanzia saa 11.00 (17h00) jioni kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabo, mjini Uyo katika Jimbo la Akwa Ibom. Muda huo uko mbele kwa saa mbili kamili kwa maana hiyo Taifa Stars itacheza dhidi ya Nigeria saa 9.00 alasiri (15h00).
    Taifa Stars iliyoondoka Dar es Salaam, Tanzania jana alfajiri, na wachezaji 18 kabla ya kuungana na Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta nchini Nigeria, ilitua salama mjini Uyo ambako imefikia Hoteli ya Le Meridien Ibom & Golf Resort. Samatta - Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea timu ya Genk ya Ubelgiji ya jijini Brussels.
    Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini utakuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.
    Wachezaji waliopo na Stars NIgeria ni makipa Said Kipao – JKT Ruvu, Aishi Manula – Azam FC, Mabeki; Vicent Andrew, Mwinyi Hajji Mngwali (wote Yanga SC), Mohamed Hussein 'Tshabalala' (Simba SC), Shomari Kapombe na David Mwantika (wote Azam FC).
    Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Shiza Kichuya (Simba SC), Ibrahim Jeba (Mtibwa Sugar), Jonas Mkude (Simba SC), Muzamil Yassin (Simba SC), Juma Mahadhi (Yanga SC) na Farid Mussa (Tenerif, Hispania)
    Washambuliaji ni Simon Msuva (Yanga SC), Jamal Mnyate, Ibrahim Ajib (Simba SC), John Bocco (Azam FC) na 

    Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS TAYARI KUUA TAI MKUBWA WA NIGERIA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top