• HABARI MPYA

    Tuesday, April 14, 2020

    VITA DHIDI YA VIRUSI VYA CORONA; TFF YAWAPIGA ‘STOP’ WAANDISHI WA HABARI KUKANYAGA KARUME

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limepiga hatua zaidi katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona baada ya kusitisha mikutano yake na Waandishi wa Habari ambayo imekuwa ikifanyika kila wiki kwenye ofisi zake zilizopo Uwanja wa Karume Ilala Jijini Dar es Salaam.
    Taarifa ya TFF imesema kwamba kuanziia sasa watakuwa wakiwasiliana na vyombo vya Habari kwa kwa taarifa maalum kuhusu mambo yake mbalimbali , hiyo kama sehemu ya tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19) unaoitikisa dunia kwa sasa.
    Na hatua hiyo inakuja siku chache baada ya TFF kuzuia kuanzia watu kufika kwenye ofisi zake, Uwanja wa Karume na kuwataka wafanye mawasiliano kwa njia ya simu watakapohitaji huduma za shirikisho hilo.
    Hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema kwamba mustakabli wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utaamuliwa na vikao maalum iwapo janga la maambukizi ya virusi vya corona litaendelea.
    Kidau alisema kwamba kama janga la COVID 19 litaendelea, msimu huu utategemea maamuzi yatakayofanywa na vyombo vinavyosimamia na kuendesha Ligi Kuu kwa pamoja na Kamati ya Utendaji ya TFF.
    Kidau alisema bado ni mapema mno kusema wamefuta msimu pamoja na kwamba msimu unaweza kwenda hadi mwishoni mwa mwezi Juni 31.
    Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
    Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon ambazo pia zimeahirishwa kwa sababu ya COVID 19.
    Kwa ujumla CAF ilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi vya corona hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VITA DHIDI YA VIRUSI VYA CORONA; TFF YAWAPIGA ‘STOP’ WAANDISHI WA HABARI KUKANYAGA KARUME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top