• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 03, 2020

  SIMBA SC YAWASHITUKIA WATU WANAOSAINI MIKATABA KWA NIABA YA KLABU BILA KUPEWA RUHUSA

  Na Mwandishi Wetu, DARES SALAAM
  UONGOZI wa Simba umesema kwamba haujatoa mamlaka kwa mtu yoyote au kundi la watu kuingia makubaliano au kusaini mikataba  kwa niaba ya klabu. 
  Taarifa iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Senzo Mbatha Mazingisa mapema leo Jijini Dar es Salaam imesema kwamba mikataba na makubaliano yote yanayohusu klabu hiyo ni lazima yasainiwe katika ofisi zao tu.
  “Imefahamika kwamba kuna baadha ya watu, makundi ya watu wamekuwa wakiingia makubaliano, mikataba na taasisi, kampuni nyingine wakijiwasilisha kama wafanyakazi, wawakilishi wa Kampuni ya Klabu ya Simba,”amesema Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Senzo Mbatha Mazingisa na kuongeza;
  “Tunapenda kuujulisha umma kuwa, Simba haijatoa mamlaka kwa mtu yoyote au kundi la watu kuingia makubaliano au kusaini mikataba  kwa niaba ya Simba. Pia umma unajulishwa kuwa mikataba na makubaliano yote yanayohusu Simba ni lazima yasainiwe na Simba katika ofisi zetu,”.

  Adha, Mtendaji huyo Mkuu wa Simba SC, Mazingisa ambaye ni raia wa Afrika Kusini amesema klabu inatoa rai kwa umma kuchukua tahadhari na watu au makundi ya watu wanaojiwasilisha kama wafanyakazi, wawakilishi wa klabu kwa ajili ya manufaa yao binafsi. 
  “Simba inakemea vikali vitendo vya namna hii na inaomba wananchi kutoa taarifa za watu au makundi ya watu wa namna hii kupitia ofisi ya Mtendaji Mkuu,”ameongeza Mazingisa, mwenye uzoefu wa kufanya kazi na klabu kubwa kama Orlando Pirates FC, Platinum Stars za kwao za kampuni ya Ligi ya Afrika Kusini (PSL).
  Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC ipo chini ya Mwenyekiti, Mohamed ‘Mo’ Dewji, Makamu wake, Salum Abdallah Muhene ‘Try Again’ na Wajumbe Hussein Kitta Mlinga, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Suleiman Haroub Said, Asha Ramadhani Baraka na Mwina Mohammed Kaduguda, ambaye pia ni kaimu Mwenyekiti wa klabu baada ya kujiuzulu Swedy Nkwabi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAWASHITUKIA WATU WANAOSAINI MIKATABA KWA NIABA YA KLABU BILA KUPEWA RUHUSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top