• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 15, 2020

  SIMBA SC YAMSHITAKI MWAKALEBELA TFF KWA KUJIGAMBA AMEZUNGUMA NA CHAMA KINYUME CHA SHERIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  KLABU ya Simba imewasilisha malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) dhidi ya Makamu Mwenyekiti wa mahasimu wao, Yanga SC, Fredrick Mwakalebela kwa kujigamba amefanya mazungumzo na mchezaji wao, Clatous Chama kinyume cha sheria.
  Taarifa ya TFF kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba Simba SC, mabingwa mara mbili mfululizo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wamelalamikia kitendo cha Mwakalabela kwamba ni ukiukaji wa Kanuni za usajili.
  “Simba imewasilisha malalamiko kufuatia kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Young Africans, Fredrick Mwakalebela kuwa wamefanya mazungumzo na mchezaji Clatous Chama wakati akiwa ndani ya mkataba, kitendo ambacho imedai ni ukiukaji wa Kanuni za usajili,” imesema taarifa ya TFF na kuongeza;
  “Katika malalamiko hayo, Simba imeomba ichukuliwe hatua kali ili kulinda kanuni zinazotawala mpira wa miguu pamoja na weledi. Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepeleka malalamiko hayo kwenye kamati yake ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambacho ndicho chombo chenye mamlaka ya kusikiliza shauri hilo,”.
  Juzi Mwakalebela alikaririwa na vyombo vya Habari akisema Yanga inamhitaji na imefanya naye mazungumzo kiungo Mzambia wa Simba SC, Chama ambaye amebakiza miezi sita katika mkataba wake.   
  Hata hivyo, baada ya kushutumiwa vikali na Msemaji wa SImba SC, Mwakalebela jana aliomba radhi na kusema kwamba kauli zake zilikuwa za utani kwa sababu klabu hizo ni watani wa jadi, ingawa hiyo haikuwazuia wapinzani wao wa jadi kupiga hatua mbele.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMSHITAKI MWAKALEBELA TFF KWA KUJIGAMBA AMEZUNGUMA NA CHAMA KINYUME CHA SHERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top