• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 17, 2020

  KOCHA AZAM FC ASHAURI IDADI YA WACHEZAJI WA KUBADILI KUONGEZWA HADI WATANO LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa klabu ya Azam FC, Aristica Cioaba, amelishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuongeza idadi ya wachezaji wa akiba kutoka watatu hadi watano.
  Cioaba ametoa ushauri huo kwa TFF, akiwa na malengo ya kuwasaidia wachezaji kujiepusha na majeraha, endapo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itarejeshwa hivi karibuni.
  Ligi hiyo kwa sasa imesimamishwa kwa muda wa mwezi mmoja tokea Machi 17 mwaka huu, kutokana na janga la ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) linaloendelea kuitesa dunia, lakini mpaka sasa haijajulikana kama itarejea baada ya muda huo wa mwezi mmoja kuisha.
  Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon ambazo pia zimeahirishwa kwa sababu ya COVID 19.
  Kwa ujumla CAF ilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi vya corona hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA AZAM FC ASHAURI IDADI YA WACHEZAJI WA KUBADILI KUONGEZWA HADI WATANO LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top