• HABARI MPYA

  Jumatatu, Aprili 27, 2020

  KELELE ZA MPIGA KELELE AMBAYE HAONEKANI KATIKA SOKA LETU

  Na Dominick Salamba, DAR ES SALAAM
  BAADA ya kufungua macho yangu na kuianza asubuhi yangu ya jumatatu hii, hakika ilikuwa asubuhi yenye staili ya kipekee kabisa.
  Niliwaza mambo mengi huku nikitafakari kile kinachoendelea Duniani kote juu ya hili janga la Corona,sikuishia hapo nikawaza kwa namna tunavyoendelea kukosa burudani za soka kila wikiendi na zile za kati ya wiki,ila mwisho wa siku nikajifariji kwakuwa afya ni zaidi ya chochote.
  Ilinibidi kuamka na kuachana na shuka lililokuwa likiniingiza kwenye limbi zito la mawazo.
  Turudi kwenye mada yetu, kwenye hoja yetu  sidhani kama kuna mtu anaweza kupinga hili pale tunapo wazungumzia wadogo zetu kina Baraka Majogoro, Zawadi Mauya, Yassin Mustapha, Yussuf Mhilu, Marcel Kaheza, Jaffar Kibaya, Hassan Kibailo na wengineo, msimu huu walikuwa kwenye kiwango bora kabisa.

  Hakika wamezisaidia sana timu zao,hakika walistahili kuvaa jezi za timu zao na kuwa sehemu ya vikosi vya kwanza vya timu zao,wamepambana mno na kwenye hilo hakuna ubishi, na kama unakubaliana na mimi, basi endelea kufuatilia nilichokuandalia leo.
  Kila nchi ina sera yake ya namna ambavyo inaendesha mpira wake lakini wakati huo kukiwa na muongozo mmoja ambao kila anayeendesha mpira kwenye nchi yake anapaswa kuufuata na si vinginevyo,na muongozo wenyewe ni ule unaotolewa na shirikisho lenye mpira wake duniani yaani FIFA.
  Shirikisho hilo lina taratibu zake ambazo ni lazima zifuatwe na wanachama wake, lakini bado kila mwanachama wa Fifa ana uwezo wa kutunga kanuni ndogo ndogo kulingana na mazingira ya nchi husika mambo kama mfumo wa ligi,usajili,ratiba ya mashindano na kanuni zingine zinazo husu mashindano. 
  👉👉Hapa ndipo panaponifanya nawaza sana hasa ninapokumbuka viwango bora vya kina Majogoro walivyoonyesha msimu huu,napata wakati mgumu sana kulikubali hili ambalo kila uchwao linaibuka na kupotea kana kwamba kuna kikundi cha watu kinachotumwa kufanya ushawishi wa jambo lenyewe na wakikosa sapoti hukaa kimya na kuibuka wakati mwingine.
  🤏🏾Moja ya vipengele ambavyo FIFA hawawezi kujaribu kupoteza muda wao kufuatilia ni idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kushiriki ligi ya nchi yoyote ile, Mfano mzuri ni kwa sisi watanzania tulianzia kwenye wachezaji watatu tu wa kigeni,tukaja kwenye kusajili watano alafu wacheze watatu,na sasa tupo kwenye wachezaji kumi na wanacheza wote inategemea na mahitaji ya mwalimu wa timu husika na mipango yake.👆
  👉🏽👉🏽Kutokana na hili la wachezaji kumi uku wakitumika wote hivi sasa kumekuwa na kelele zisizojulikana zinatoka wapi, mpaka sasa hatujui kama ni msimamo wa  Serikali kupitia waziri mwenye dhamana na michezo au shirikisho la mpira wenyewe au vilabu vinavyoshiriki ligi kuu kuwa pengine ndio wenye hizi kelele ambazo uwa zinakuja na kupotea uku mwenye kelele hasa akiwa hajulikani yupo wapi na anasimama na hoja gani nzito juu ya hili.
  Kwenye mpira wetu au ndio tutauzamisha kabisa mpira wetu ambao unaonekana kusogea kwa kiasi fulani ukilinganisha na miaka 15 nyuma,sitaki kuamini kuwa nchi yenye ligi ya Timu 20 ambazo zinaruhusiwa kusajili wachezaji 30 kwa kila timu na kupelekea kuwa na jumla ya wachezaji 600 katika ligi kuu huku wachezaji wa kigeni wakiwa hawazidi 50 alafu bado ionekane wapo wengi na wanachangia kufifisha soka letu sitaki kuliamini hili.
  👉🏽👉🏽Wakati nikiwaza zile pesa wanazolipiwa wachezaji wa kigeni ili kupata vibali vya kucheza soka hapa kwetu,achana na mzunguko wa kifedha kutokana na uwepo wao hapa kwetu mbali na kuwa kama sehemu ya kulitangaza Taifa letu duniani kote.
  Kabla hujanipa jibu la tafakari yako kuhusu jambo hili, nakupeleka kidogo pale Congo, hapa ndipo tunapoweza kujifunza kwa mfano halisi na unaoishi.
  Wakongomani waliamua kuondoa vikwazo kama hivi ambavyo waligundua kuwa havitausaidia mpira wao kwenye harakati za kutoka sehemu moja ya kimaendeleo kwenda kwingine, wao wakaamua kwenye mpira wao kusiwe na idadi ya wachezaji wa kigeni,timu zisajili tu kadri zinavyoweza ikibidi timu nzima iwe na wageni watupu, tujiulize kitu kimoja,tunadhani Kongo wakifanya maamuzi hayo hapakuwa na wachezaji wazawa? Nani asiyemjua Tresso Mputu? Deo Kanda? Makusu Mundele? au yule kipa mwenye rikodi zake yaani Kidiaba!! na wakongomani wengine kibao wanaocheza soka la kulipwa barani ulaya,wenzetu walikataa kuwalemaza wachezaji wao wakiamini kuwa uwepo wa wachezaji wa kigeni kutawapa changamoto na kujituma zaidi ili kufika mbali katika maslahi yao pamoja na ya Taifa kwa ujumla.
  Waliamini kuwa kama wewe ni raia wa Kongo na unautaka kweli mpira basi ni lazima upambane, utaonandogondogo Afrika utawakuta wapo wa kutosha.
  🤜🏿🤜🏿Baada ya kupata jibu la tafakuri yako na mfano hai niliokupa kuhusu Wakongomani njoo sasa tujadili yanayotuhusu.
  Kwangu mimi jambo baya kabisa katika maisha ni kuamua kwenda kusikojulikana huku ukiamua kujificha kwenye kivuli cha ule msemo wasemao waswahili kuwa maisha ni popote, ni kweli inaweza kuwa hivyo lakini hupaswi kuamini sana anachokisema mswahili, uhitaji sababu nyingine yoyote ya kutokumuamini isipokuwa maneno yake mengi, ukweli ni kwamba tunahitaji vijana wetu wapate nafasi ya kucheza mda mwingi, lakini sababu kubwa ya mahitaji yetu ni kupata timu bora kabisa ya taifa,sidhani kama hilo tutalifikia kwa kuwapunguza wachezaji wa kigeni ili tu vijana wetu wacheze, kama ni kweli tunataka timu bora ya taifa tuweke misingi imara ya kuwandaa wachezaji tangu wakiwa watoto ili waweze kumudu vizuri soka la ushindani linaloendelea kwa kasi kubwa sana,kama wachezaji wetu wanataka kucheza basi washindane na wageni ili kupata nafasi ya kucheza na si kuwabeba kwa kuwaondoa wageni,hatutofika popote.
  Ngoja nikupe mfano ulio hai , pale simba walisajili mtu kweli kweli kwenye eneo la kiungo mkabaji,nani asiyemkumbuka James Kotei? Pamoja na ubora wake wote lakini bado Jonas Mkude Alipata nafasi ya kucheza na kuwafanya baadhi ya makocha kuhama kwenye staili ya kutumia kiungo mmoja mkabaji na kujikuta wanawatumia wote(double pivot), akaja Gerson Fraga lakini Mkude bado anaonekana kuwa vizuri zaidi,Mkude huyu kwa nini asikusaidie kwenye timu ya taifa?
  Pale Yanga wakati Simon Msuva yupo alicheza mbele ya wachezaji wa kulipwa na wenye majina makubwa, ilikuwa Yanga yenye ushindani mkubwa sana, Donald Ndondo Ngoma(DNN), Obrey Chora Chirwa (OCC) pamoja na Amisi Tambwe lakini bado Simoni Msuva alipenya na kukiwasha vibaya mno pale Yanga na leo wote ni mashahidi mahali alipo Msuva na bado anaendelea kukaza buti katika soka la ushindani.
  Kama tutaufurahia ubora ulioonyeshwa na kina Baraka Majogoro, Mauya Gift, Yasini Mustapha, Kaheza, Kibaya,Mwashilindi na wengineo na kudhani njia salama ya kuwabakisha kwenye ubora wao ni kuwaondoa wachezaji wa kigeni basi tutakuwa tunafeli mno,badala yake ni kuhakikisha tunabadili mitazamo ya hawa vijana lazima wawe na njaa ya mafanikio,lazima wamtamani Mbwana samatta na pengine wawaze zaidi ya Samatta ,lakini kama watazawa kununuliwa Toyota brevis,kupangiwa nyumba Tabata na kuandikwa kwenye magazeti yetu kwa usajili wa milion 20,30 au 50 kwa mikataba ya miaka 2  basi hata tuwaondoe wageni wote hakuna tutakapo fika.
  Tunapaswa kujua kuwa ubora walionao vijana wetu kwa sasa umechangiwa kwa kiasi kikubwa mno na uwepo wa wachezaji wa kigeni kwenye ligi yetu, anachokifikiria Iddi Mobi au Nondo Mwamnyeto kuelekea kwenye mchezo dhidi ya simba ni namna ambavyo wanaweza kumdhibiti Meddie Kagere,Kahata au Mikissoni, wachezaji wa viwango vya juu mno ambao kama tutawapunguza au kuwaondoa kwenye ligi yetu basi moja kwa moja tutamuathiri Mobi na wenzake na kujikuta tunayumba sana,Mwamnyeto huyu anayeshindana na kina Kagere na Morisson kwa nini asiwe bora? wakati anashindana na wachezaji wenye ubora mkubwa?
  Tusiwe watu wa kuishi kwa tafakari nyepesi,tusitafute majibu mepesi kwa maswali magumu hakuna njia ya mkato katika hili lazima tukubali kutengeneza misingi soka lianzie chini,tupate vituo vingi vya kukuza vijana wetu,tupate waalimu wengi kwenye soka la vijana ambao wamesoma mtaala mmoja tena katika vyuo vinavyotambulika na ziwe kozi za muda mrefu sio hizi za wiki tatu hapo tutasogea kwelikweli.
  Ila kuendelea kumpigia debe Kichuya acheze mbele ya ubora walio nao Mikisson,Kahata na Kanda au Rafael Daudi acheze mbele ya Niyonzima,huku Dante acheze mbele ya Lamine kisa utanzania wake si kuwajenga vijanja wetu ila ni kuwapoteza,njia pekee ya kuwasaidia ni kuwaambia wajitume zaidi na kuwashawishi waalimu wao kwani hakuna mwalimu anayependa kupoteza mechi.Wote tunakumbuka kiungo wa Yanga Feisal Salumu alikuja vizuri alafu akapotea na ameongeza bidii leo hii anapata nafasi mbele ya Viungo wa kigeni kwa anafanya kazi ya maana uwanjani.
  Asanteni sana na tuendelee kuwa makini maana Korona ipo na inazuilika,tuendelee kuchukua tahadhali, tukutane wiki ijayo.

  (Dominick Salamba ni mchambuzi wa soka anapatikana pia kupitia katika Akaunti yake ya instagram kama @dominicksalamba au namba ya simu)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KELELE ZA MPIGA KELELE AMBAYE HAONEKANI KATIKA SOKA LETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top