• HABARI MPYA

    Friday, April 03, 2020

    YANGA SC YAWATEUA MWAITENDA NA BATENGA KUWA WAJUMBE WAPYA WA KAMATI YA UTENDAJI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa Yanga umewateua Qs. Suma Mwaitenda na Haroun Batenga kuwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kuziba nafasi za Wajumbe wawili waliojiuzulu mwishoni mwa mwezi uliopita.
    Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC leo Jijini Dar es Salaam, imesema kwamba uamuzi huo umefuatia kikao cha Kamati ya Utendaji, chini ya Mwenyekiti Dk. Mshindi Mbette Msolla kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) wa Katiba ya klabu hiyo.
    Aidha, taarifa hiyo imesema kwamba Kamati ya Utendaji imemteua Hamad Islam kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, wakati Dominic Albinus anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi. 
    Qs. Suma Mwaitenda (kulia) ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC

    Wajumbe wa kuteuliwa waliojiuzulu mwishoni mwa mwezi uliopita ni Shijja Richard na Said Kambi na mmoja wa kuchaguliwa, Rodgers Gumbo, hivyo kufanya jumla wa Wajumbe watano wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC waliong’atuka na kusimamishwa Machi.
    Ikumbukwe baada ya kikao chake cha Machi 26 na 27, mwaka huu Kamati ya Utendaji ya Yanga SC iliwasimamisha wajumbe wake wawili, Salim Rupia na Frank Kamugisha hadi hapo mkutano mkuu utakapofanya maamuzi kwa mujibu wa katiba.
    Kamati ya Utendaji ya Yanga iliyoingia madarakani Mei 5, mwaka jana ilichukua hatua hiyo kufuatia kutokea sintofahamu iliyosababisha mdhamini wa klabu, Kampuni ya GSM kusitisha kutoa misaada iliyo nje ya mkataba wake.
    Sasa Kamati ya Utendaji Yanga inaundwa na; Mwenyekiti Dk. Msolla, Makamu Mwenyekiti, Frederick Mwakalebela na Wajumbe Hamad Islam, Mhandisi Bahati Faison Mwaseba, Dominick Ikute, Arafat Haji na Saad Khimji wa kuchaguliwa na Dk. Athumani Kihamia, Qs. Suma Mwaitenda na Haroun Batenga wa kuteuliwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAWATEUA MWAITENDA NA BATENGA KUWA WAJUMBE WAPYA WA KAMATI YA UTENDAJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top