• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 09, 2020

  GSM YAREJESHA AMANI YANGA BAADA YA KUSEMA ITAENDELEA KUISAIDIA KLABU NDANI NA NJE YA MKATABA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMPUNI ya GSM imesema itaendelea kuisaidia Yanga SC nje ya makubaliano ya kimkataba ili kuhakikisha inakuwa moja ya klabu kubwa Afrika.
  Hayo yalisema jana na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said wakati wa mkutano wa pamoja na Mwenyekiti wa Yannga SC, Dk.Mshindo Msolla na vyombo vya Habari jana.
  Hersi aliyataja maeneo watakayojikita zaidi nje ya mkataba wao wa udhamini ikiwemo kulipa mishahara ya wachezaji, posho, masuala ya ufundi, Uwanja, usajili na mchakato wa mabadiliko kuelekea mfumo wa kisasa wa uendeshaji.
  Na hatua hiyo inafuatia uongozi wa Yanga kuwasimamisha Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliokuwa wanatilia shaka ufadhili wa GSM kiasi cha kampuni hiyo kutangaza kusitisha misaada iliyo nje mkataba wa udhamini wao wa vifaa vya michezo.
  Hali ya hewa ilichafuka Yanga baada ya GSM kutangaza kusitisha misaada iliyo nje ya mkataba kufuatia kupoteza imani na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.
  Hata hivyo, mambo yalikaa sawa baada ya Wajumbe hao kujiuzulu kwa shinikizo la wapenzi na wanachama na wengine kusimamishwa.
  Wajumbe wa kuteuliwa waliojiuzulu mwishoni mwa mwezi uliopita ni Shijja Richard na Said Kambi na mmoja wa kuchaguliwa, Rodgers Gumbo, hivyo kufanya jumla wa Wajumbe watano wa Kamati ya Utendaji ya Yanga SC waliong’atuka na kusimamishwa Machi.
  Ikumbukwe baada ya kikao chake cha Machi 26 na 27, mwaka huu Kamati ya Utendaji ya Yanga SC iliwasimamisha wajumbe wake wawili, Salim Rupia na Frank Kamugisha hadi hapo mkutano mkuu utakapofanya maamuzi kwa mujibu wa katiba.
  Sasa Kamati ya Utendaji ya Yanga iliyoingia madarakani Mei 5, mwaka jana inaundwa na; Mwenyekiti Dk. Msolla, Makamu Mwenyekiti, Frederick Mwakalebela na Wajumbe Hamad Islam, Mhandisi Bahati Faison Mwaseba, Dominick Ikute, Arafat Haji na Saad Khimji wa kuchaguliwa na Dk. Athumani Kihamia, Qs. Suma Mwaitenda na Haroun Batenga wa kuteuliwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: GSM YAREJESHA AMANI YANGA BAADA YA KUSEMA ITAENDELEA KUISAIDIA KLABU NDANI NA NJE YA MKATABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top