• HABARI MPYA

  Thursday, April 30, 2020

  TUKIWAPA THAMANI WACHEZAJI WETU, WATAFANYA MAKUBWA

  Na Ibrah Mkemia, DAR ES SALAAM
  NIANZE kwa kuliombea na kulitakia afya njema  Taifa langu la Tanzania,  Taifa ambalo lina watu wakarimu na wenye busara, amani, na upendo. Tukiwa bado tunaendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa hatari wa corona, yapo mambo mengi ambayo kama wanamichezo wapenda burudani ya mpira wa miguu tunapaswa kujadili kwa kina ili kuweza kupata mawazo chanya kama sio muarubaini kabisa.
  Kipindi hiki ambapo kuna mengi magumu tunayapiti lakni kwa uwezo wa Mungu naimani yatapita na Taifa litaendelea kubaki kama Taifa lenye malengo, matumaini ya kufika katika uchumi wa kati wa viwanda. Kama kaulimbiu ya Mheshimiwa Rais kwamba Tanzania iwe nchi ya viwanda. Na kiwanda kimoja wapo kipo kwenye michezo nacho ni mpira wa miguu (kandanda).

  Maswali mengi ya watanzania, wapenda michezo yamekuwa yakiuliza ni kwanini tumekuwa na hatua za mtoto mdogo katika kuyatafuta mafanikio na sio hatua za mtu mzima hususani katika swala la michezo. Hili limekuwa gonjwa sugu ambalo dawa yake bado iko maabara na hatujui ni lini chanjo yake itaanza kijaribiwa. 
  Kumekuwa na mijadala mingi ndani ya Taifa letu kuhusu wanasoka (wachezaji) wetu wa sasa na wa zamani kutopewa heshima yao katika taifa hili. Sasa ni wakati sahihi kwa wadau na wanamichezo kujikita katika mjadala huu kwa makini. Kwani waswali wanasema "Mcheza kwao hutunzwa".
  Hivi karibuni alisikika kiongozi mmoja ndani ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) akisema " Timu ili kuweza kuwa na haki ya kucheza kwenye ligi kuu ni lazima ihakakikishe imelipa wafanyakazi wake kwa maanna wachezaji pamoja na makocha stahiki zao yakiwemo madeni yote ya nyuma". 
  Ukiwa kama mdau wa michezo na mpenda mafanikio ya soka la Tanzania naimani utakuwa umekubaliana na kauli hiyo. Hili ni jambo jema sana kwa wanasoka wote popote walipo. Kwani wamesaidiwa jukumu la kukumbushia madeni yao ili walipwe ndani ya muda sahihi.
  Swala linabaki kwa mchezaji mwenyewe,  Mchezaji anapaswa kutambua kuwa yeye ni bidhaa amabayo inatembea na inaonekana kirahisi. Hivyo kama yeye ni bidhaa anapaswa kujiweka na kujitunza katika thamani halisi,  Na kujitambua hivi sasa kuwa yeye ni nani na anataka nini? Na ana malengo gani katika soka lake.
  Asilimia kubwa sana ya wachezaji wa kitanzania wanacheza katika timu kwa kukopwa. Na inafikia hatua mchezaji anacheza kwa mrefu bila kupewa stahiki zake. Na huu pia ni mjadala mwengine ambao unaitajika muda kuweza kuuzungumzia. Mikataba ya wachezaji imekuwa siri, wachezaji wengi hawawezi kutafsri mikataba,  na waajiri wanalijua hilo lakini kutokana na kutothamini wachezaji wazawa basi wanamsainisha tu. Hii inatia simanzi sana kwenye soka letu. Waswahili wanasema "Tikiti baya liko shamabani mwako".
  Nasikitika sana kuona wanasoka wengi wa zamani na hata wa sasa wakiwa na hali mbaya kiuchumi. Sio kama nakashifu ila nikikumbuka walivyolitendea taifa hili makubwa katika upande wa michezo hasa kwa ngazi ya vilabu binafsi sioni sababu ya wao kuwa katika hali hii. Juhudi nyingi zinafanywa na chama kinachojihusisha na kusimamia haki zote za wachezaji (Spotanza). Kuweza kuweka mambo sawa pindi yanapoonekana yanakwenda ndivyo sivyo hongera kwao.
  Wanafanya kazi kubwa sana kuweza kuwaelimisha wanchama wao ambao ni wachezaji ili waweze kuepuka migogoro ya kimikataba baina yao na waajiri wao ambao ni timu husika. "Wachezaji someni mikataba msitikiswe kama kiberiti na pesa za ubaoni, ahadi zisizo tekelezeka wakati wa kipindi cha usajili.  "Spotanza mnafanya kazi kubwa sana kama hamtoonekana leo basi hata kesho kwa Mungu mtakuta pongezi yenu. Mungu akupe maisha marefu Mussa Kisoki.
  Pia kwa upande wa vilabu hapa kuna tatizo napo, sijui ni mazoea au kukosa weledi au ndo tuseme hawana mipango thabiti kwenye chaguzi zao. Utakuta wanaweka viongozi vizuri sana kama mwenyekiti, na hata zile kamati za utendaji. Shida inakuja wakati wa utekelezaji wa nafasi ya mmoja mmoja katika majukumu yao ya kila siku. Unajiuliza kweli vilabu vyetu vina mpango endelevu kiuchumi, au ndani ya timu kuna hao wanaojiita wachumi kweli?
  Hivi karibuni tumeshuhudia vilabu vinapata hasara kubwa kwa kutotumia watu kama hawa ili kuweza kujifanikisha kimaendeleo. Tumeshuhudia vilabu vikiingia mikataba na wachezaji pamoja na makocha. Alafu ndani ya muda mfupi tunasikia wameachana na watu hao huku kukiwa na madeni ya mishahara na stahiki nyingine kwa waajiriwa hao, Na timu bado inaendelea kufanya usajili ndani ya kipindi hiko hiko tena kwa pesa kubwa kuliko.  Ifikie hatua tujiulize tunataka maendeleo katika vilabu vyetu au tunataka kuwashushia thamani wachezaji wetu.
  Hatuhitaji Nabii wala mwanasayansi aje atukumbushe kuwa bado tuko nyuma sana na tunahitaji kuamka usingizini. Kila mtu atambue umuhimu wake katika nafasi yake. Kama ni mchezaji basi acheze bila kuwa na kikwazo cha mshahara wala mahitaji yake muhimu na kama ni kiongozi ahahakishe anaendesha kiwanda ambacho ndani yake kuna wafanyakazi wengi ambao ni nguvu kazi ya Taifa. "Kiongozi katika sekta ya maendeleo uliyopewa dhamana onesha kipi kimekuweka hapo "Mawazo bila ufumbuzi ni ujinga"
  Tusipige hatua moja mbele alafu tukarudi tano nyuma tutakuwa hatujafanya kitu. Tukiwapa thamani wachezaji wetu leo na wakawa na maisha mazuri. Watakuwa kioo kizuri kwa vijana wetu wanaochipukia kwani watatamani mafanikio yao. Na njia peke ya kuyapata ni kusukuma gozi la ng'ombe. 
  Kila nyumba ya Mtanzania ina kipaji cha mpira ila je? Tumejipanga kuwapokea kikamilifu au na wao tutawapa mikataba ya kuwakopa kama mababu zao na baba zao. Tusisahau kwamba "Tusipoziba ufa tutajenga ukuta".
  (Imeandikwa na Ibrah Mkemia anayepatikana kwa barua pepe; kalomoibrahim@gmail.com au nambari za simu +255 715 147 449 na +255 692 945 323)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUKIWAPA THAMANI WACHEZAJI WETU, WATAFANYA MAKUBWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top