• HABARI MPYA

  Jumamosi, Agosti 24, 2019

  YANGA SC YAICHAPA TOWNSHIP ROLLERS 1-0 NA KUBISHA HODI MAKUNDI LIGI YA MABINGWA

  Na Mwandishi Wetu, GABORONE
  TIMU ya Yanga SC imefanikiwa kwenda hatua ya mwisho wa mchujo wa kuwania kuingia kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa ugenini wa 1-0 dhidi ya Township Rollers Uwanja wa Taifa mjini Gaborone, Botswana.
  Kwa kwa matokeo hayo, Yanga SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza wiki mbili zilizopita mjini Dar es Salaam na itamenyana na Zesco United ya Zambia iliyoitoa Green Mamba ya Eswatini kwa jumla ya mabao 5-0, ikishinda 2-0 ugenini na 3-0 nyumbani.
  Shujaa wa Yanga SC leo ni mshambuliaji mpya, Mganda Juma Balinya aliyefunga bao hilo pekee kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 41.
  Mshambuliaji Mganda Juma Balinya (kulia) ameifunga bao pekee Yanga leo ikiitoa Township Rollers

  Lakini pia sifa zimuendee mlinda mlango, Metacha Boniphace Mnata ambaye pamoja na kuokoa michomo mingi kwa ujumla – alidaka na mkwaju wa penalti wa mshambuliaji wa Township Rollers, Segolame Boy dakika ya 63.
  Penalti hiyo ya utata ilitolewa na baada ya kiungo Mkongo wa Yanga SC, Papy Kabamba Tshishimbi kuondosha mpira miguuni mwa Tlhalefo Molebatsi na kuonekana kama alimgusa mchezaji huyo wa wenyeji aliyekuwa anatafuta nafasi ya kupiga.
  Kwa ujumla haukuwa ushindi mwepesi kwa Yanga SC, kwani wenyeji walitengeneza nafasi nyingi nzuri, ila utulivu wa safu ya ulinzi ya Yanga na haswa kipa uliwanyima mabao.
  Kwa dakika zote 20 za mwisho kipa Mnata aliyesajiliwa kutoka Mbao FC ya Mwanza alikokuwa anacheza kwa mkopo kutoka Azam FC iliyomuibua kupitia akademi yake alicheza anachechemea baada ya kuumia katika moja ya jitihada zake za kuokoa.

  Kwenye Raundi ya pili, Yanga SC wataanzia nyumbani tena kati ya Septemba 13 na 15, kabla ya kusafiri kwenda Zambia kwa mchezo wa marudiano kati ya Septemba 27 na 29.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Paul Godfrey, Ally Mtoni ‘Sonso’, Lamine Moro, Kelvin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Mapinduzi Balama/Mrisho Ngassa dk77, Mohammed Issa ‘Banka’/Feisal Salum ‘Toto’ 70, Sadney Urikhob, Juma Balinya/Raphael Daudi dk85 na Patrick Sibomana.
  Township Rollers; Wagarre Dikago, Kamogelo Matsabu, Ofentse Nato, Thatayaone Ditlhokwe, Galabgwe Moyana, Maano Ditshupo/Jackson Lesole dk74, Mothusi Cooper, Segolame Boy, Motsholetsi Sikele/Kitso Mpuisang dk82, Tumisang Orebonye na Phenyo Serameng/Tlhalefo Molebatsi dk61.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAICHAPA TOWNSHIP ROLLERS 1-0 NA KUBISHA HODI MAKUNDI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top