• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 15, 2019

  AZAM FC YAWAPA ONYO SIMBA SC MECHI YA NGAO, YAWAPIGA NAMUNGO 8-1 LEO CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KATIKA kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii, timu ya Azam FC leo imeichapa mabao 8-1 Namungo FC ya Ruangwa mkoani Lindi katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Azam FC, washindi wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) watamenyana na mabingwa wa Ligi Kuu ya nchi, Simba SC Jumamosi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa Ngao ya Jamii.
  Na kuelekea mchezo huo maalum kuashiria upenuzi wa pazia la msimu mpya, Azam FC leo imeishushia kipigo kikali Namungo iliyopanda Ligi Kuu.

  Mabao ya Namungo leo yamefungwa na Muivory Coast, Richard Djodi, Iddi Suleiman ‘Nado’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Bruce Kangwa, Shaaban Iddi ‘Chilunda’, Obrey Chirwa, Abal Kassim Khamis na Iddi Kipagwile.
  Simba SC ndio wanashikilia Ngao ya Jamii baada ya kuichapa Mtibwa Sugar 2-1 msimu uliopita Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Agosti 18, mwaka jana.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Elly Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma wote wa Dar es Salaam, na Ferdinand Chacha wa Mwanza, mabao ya Simba SC yalifungwa na mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere dakika ya 29 kiungo Hassan Dilunga dakika ya 45, wakati la Mtibwa lilifungwa na mshambuiaji chipukizi, Kelvin Sabato Kongwe au Kiduku dakika ya 33.
  Hiyo ilikuwa mara ya nne kwa Simba SC kutwaa Ngao ya Jamii, baada ya 2011 wakiifunga Yanga 2-0, 2012 wakiifunga Azam FC 3-2 na mwaka 2017 wakiwafunga tena mahasimu wao wa jadi, Yanga kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
  Azam FC yenyewe imetwaa Ngao ya Jamii mara moja tu, 2016 walipoifunga Yanga kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 2-2 kati ya mara tano ilizowania.
  2012 walifungwa 3-2 na Simba SC, 2013 walifungwa 1-0 na Yanga SC, 2014 walifungwa 3-0 na Yanga SC na 2015 walifungwa na Yanga SC kwa penalti 8-7 baada ya sare ya 0-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWAPA ONYO SIMBA SC MECHI YA NGAO, YAWAPIGA NAMUNGO 8-1 LEO CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top