• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 13, 2019

  YANGA SC KUMENYANA NA AFC LEOPARDS JUMAPILI MECHI YA KIRAFIKI SHEIKH AMRI ABEID

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Yanga SC itamenyana na AFC Leopards ya Kenya Jumapili Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha katika mchezo wa kirafiki.
  Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Frederick Mwakalebela amesema leo katika mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam kwamba maandalizi ya mchezo huo yamekamilika. 
  Utakuwa mchezo maalum wa mwisho wa kujiandaa na mechi ya marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers utakaofanyika Agosti 24 Uwanja wa Taifa mjini Gaborone.
  Na utachezwa siku mbili baada ya mchezo mwingine wa kwanza wa kirafiki, dhidi ya Polisi Tanzania Ijumaa mjini Moshi, pia kujiandaa na mechi dhidi ya Township Rollers.

  Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Frederick Mwakalebela (kulia) akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari leo 

  Yanga inayofundishwa Kocha Mkongo, Mwinyi Zahera imewasili mjini Moshi mkoani Kilimanjaro leo kuweka kambi wa kujiandaa na mchezo dhidi ya Township Rollers.
  Hayo ni mapendekezo ya Kocha Mwinyi Zahera aliyetaka timu ikaweke kambi katika mji wenye hali ya hewa ya baridi sawa na Gaborone.
  Yanga SC inahitaji ushindi wa ugenini lazima ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo, kufuatia kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani, Jumamosi iliyopita na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC KUMENYANA NA AFC LEOPARDS JUMAPILI MECHI YA KIRAFIKI SHEIKH AMRI ABEID Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top